Geita. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana nchini kutokubali kurubuniwa kwa namna yoyote kuharibu amani ya Taifa, na badala yake amewataka wawe wazalendo na kuipenda nchi yao.
Mbali na wito huo, mgombea huyo ametoa ahadi mbalimbali kwa wananchi katika Mkoa wa Geita, ambako ameanza kampeni zake za uchaguzi baada ya kuhitimisha katika Mkoa wa Shinyanga jana.
Samia ametoa rai hiyo leo, Jumapili Oktoba 12, 2025, eneo la Runzewe, wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita, katika mwendelezo wa kampeni zake za kunadi ilani ya CCM na kuomba ridhaa ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Mgombea huyo wa urais amesema kuwa ni muhimu kundi hilo kutambua umuhimu wa amani iliyopo hapa nchini, na kuwa ni moja ya jambo linalofanya Tanzania kuheshimiwa ulimwenguni.
Amewaeleza vijana kuwa nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko moja, na tangu imeundwa imepigana vita moja na Idd Amini, si kwa sababu ya udhaifu wao bali kutokana na chokozo, lakini kwa miaka yote nchi imekuwa salama na ina amani.
“Sasa ninalotaka kuwaambia vijana, naomba mnisikilize nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko moja peke yake. Toka nchi hii imeundwa tumepigana vita moja tu na Idd Amini, na kwa sababu alituchokoza si ndio, lakini miaka yote nchi hii iko salama, tuna amani,” amesema na kuongeza:
“Sisi tukiwa wadogo tulizaliwa tukakuzwa kwenye amani, tumekuwa wakubwa tunaendesha nchi hii bado tunalinda amani. Vijana, twendeni tukalinde amani yetu, tusikubali kwa hali yoyote kushawishiwa kuharibu amani yetu. Hamtakwenda kwenye kuchimba, hamtakwenda kwenye muziki, hamtafanya chochote amani ikiharibika.”
Mgombea huyo ameendelea: “Wakati nakuja huku nilisimama Kahama pale na nikafanya mkutano, Kahama pale kuna mchanganyiko wa watu kutoka nchi jirani, wote wako pale, wamefuata biashara, wamefuata maisha, wamefuata amani. Mkiharibu nyinyi kwenu, kama wale anakuja huku, nyie mtakwenda wapi? Hamna pa kukimbilia,” ameongeza.
Samia amesema hakuna pa kukimbilia nchini, hivyo kuwasihi vijana wasikubali kurubuniwa au kushawishiwa kufanya chochote cha kuharibu sifa nzuri ya nchi.
“Nchi yetu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni nchi inayoheshimiwa sana ulimwenguni kwa sifa zake, amani yake, maendeleo yake na kila kitu. Niwasihi sana vijana wangu, tuwe wazalendo, tuipende nchi yetu, tusije tukarubuniwa kwa namna yoyote ile na tukaharibu nchi yetu,” amefafanua.
Mgombea huyo amewaeleza vijana wa eneo hilo kuwa jambo la faraja linalowahusu ni ujenzi wa kiwanja cha michezo cha kisasa kinachojengwa eneo la Ushirombo kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Jambo la faraja, vijana wangu, linahusu kwamba alikuja mbunge wenu akasema vijana wangu hawana sehemu ya michezo. Tutajengwa uwanja wa kisasa, Bukombe itaingia kwenye ramani kama mechi za Ligi Kuu. Vijana, tunawapa fursa za kiuchumi na maeneo ya kufanyia michezo, Serikali tunawapenda sana na tunawaomba muipende nchi yenu,” ameongeza.
Akizungumzia sekta ya kilimo, amesema Serikali yake itaendelea kutoa ruzuku kwa wakulima, na katika wilaya ya Bukombe watajenga skimu za umwagiliaji 10 ili kulinda mazao ya mpunga, ili wakulima waendelee kulima na kuuza nje ya nchi kuongeza mapato ya Taifa.
“Wafugaji tumewaangalia kwa jicho la karibu sana, tumetoa ruzuku ya chanjo kwa wanyama wetu ili kulinda afya zao, liweze kuuza mazao ya mifugo nje ya nchi. Lazima wanyama wetu wachanjwe, lakini tumejenga majosho, machinjio ya kisasa, maeneo mnalimbali na minada pia,” amesema Samia kabla ya kuomba kura kwake, wabunge na madiwani.
Mmoja wa vijana waliojitokeza katika mkutano huo, James Israel, amesema ni muhimu vijana kuendelea kupewa elimu ya umuhimu wa kujitokeza kupiga kura ili wapate wawakilishi wanaowataka.
“Elimu zaidi itolewe kwa vijana watahamasika kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wao katika ngazi za maamuzi, kuanzia Rais, wabunge na madiwani, kwani ni haki yao ya kikatiba,” amesema.
Akiwa katika Wilaya ya Bukombe, Samia ameahidi kuendelea kuboresha na kuinua sekta ya maziwa wilayani humo ili kuinyanyua biashara ya maziwa na kuinua uchumi wa wafugaji. Pia, ameahidi kujengwa viwanda vitakavyochakata maziwa ili kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo.
Samia amesema iwapo atachaguliwa kuendelea kipindi cha pili, Serikali yake itawekeza na kuinua sekta ya maziwa ili kukuza uchumi wa wafugaji.
Amesema Serikali yake, kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo, imejipanga kuongeza nguvu kwenye sekta ya mifugo kwa ujumla kwa kutoa ruzuku ya chanjo, kujenga majosho, kukarabati minada na kujenga minada mipya pamoja na machinjio.
“Tumeamua sasa tuingie kwenye ng’ombe wa maziwa, tuinyanyue sekta ya biashara ya maziwa ambapo Bukombe ni wazalishaji wa maziwa wazuri. Tunakwenda kunyanyua sekta ya maziwa, lakini pia kuweka viwanda vitakavyochakata maziwa ili wafugaji wauze bidhaa, fedha iingie mfukoni, maisha yaendelee,” amesema.
Kuhusu madini, amesema kipindi cha nyuma baadhi ya vijana walikuwa wakienda eneo la Pori la Kigosi na kuiba madini, ila kwa kutambua utu wa vijana, alimtaka Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko, na viongozi wengine serikalini kukaa na kuangalia namna vijana hao wa Bukombe wanavyoweza kunufaika na rasilimali hiyo.
“Unapokuwa na mtoto ambaye ana tabia mbaya kidogo, mama anapopika na kufunika nyama jikoni, mtoto anakwenda kudokoa dokoa ile nyama na kula. Wazazi wengine watamchapa yule mtoto mpaka aseme ‘nimezaliwa hapa,’” amesema na kuongeza:
“Lakini wazazi wengine, nikiwemo mimi, kama mtoto ana tabia hiyo kwenye zizi, kuna ng’ombe, mbuzi, kondoo, nitachinja wanyama nipike ndani, watoto wale mpaka wakinai nitawalea namna hiyo.
“Na ndivyo nilivyofanya kwa upande wa madini. Vijana wangu wa Bukombe walikuwa wanakwenda kuniibia madini kule Kigosi, lakini rasilimali ile Mungu ameishusha hapa Bukombe. Sasa, badala ya wakaibe, wakamatwe, wapigwe na askari wa hifadhi, wapelekwe mahakamani, nikasema hapana,” amesema Samia.
Kwingineko katika Wilaya ya Mbogwe, ameahidi ujenzi wa soko la kisasa, maghala ya chakula na mradi wa maji utakaoondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa baadhi ya kata zinazokabiliwa na tatizo hilo.
Amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza kwa kipindi kijacho, atashughulikia upungufu wa maji katika baadhi ya kata wilayani humo na kuhakikisha adha hiyo inaondoka.
Hadi sasa, amesema, asilimia 86 ya wananchi wilayani humo wanapata huduma ya maji safi na salama. Akichaguliwa, atahakikisha asilimia 14 iliyosalia inapata huduma hiyo muhimu kupitia mradi wa maji wa Masumbwe kutoka Ziwa Victoria, uliofikia asilimia 68.
“Tumepiga hatua katika kufikisha huduma ya maji katika wilaya hii na tumefikisha asilimia 86, najua kuna kata ambazo zinakabiliwa na upungufu wa maji hususani kipindi hiki cha kiangazi ikiwemo kata ya Mbogwe, habari njema ni kwamba mradi wa maji wa thamani ya Sh4.3 bilioni utasaidia kumaliza tatizo hili na mradi umefikia asilimia 68,” amesema.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Anna Gabriel, amesema maboresho ya sekta ya afya yamesaidia wanawake na watoto, na kwa sasa hawafuati huduma za afya mbali na makazi yao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Awali, akina mama na watoto tulikuwa tunapata adha ya huduma ya afya, ila kwa sasa huduma hizo zimesogezwa kwenye maeneo yetu na hospitali za wilaya zimeboreshwa pia,” ameongeza.