DK.SAMIA :TUMEWEKA UTARATIBU MZURI WA UCHIMBAJI MADINI KWA WANANCHI WILAYANI BUKOMBE

 Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Geita 

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali imeamua kuweka utaratibu mzuri ambao umewezesha wananchi kushiriki uchimbqji madini katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Akizungumza katika nkutabo wa kampeni leo Oktoba 11,2025 mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Bukombe katika Uwanja wa Shule ya Msingi Bukombe mkoani Geita Dk.Samia Suluhu Hassan amesema wachimbaji wa wilaya hiyo walikuwa wakivamia Pori la Akiba Kigosi Moyowosi kuchimba madini ya dhahabu kwa njia isiyokuwa rasmi.

Amesema kwamba rasilimali hiyo Mungu ameishusha nchini iwanufaishe wananchi wakiwemo vijana  hivyo kuliko kuendelea kuiba Serikalii iliamua kuwamilikisha.

“Unapukuwa na mtoto ambaye anatabia mbaya kidogo mama anapopika na kufunika nyama jikoni, mtoto huyo anapokwenda kudokoa ile nyama sasa wazazi wengine atamchapa mtoto mpaka aseme hapa nimezaliwa.

“Lakini wazazi wengine nikiwemo mimi mtoto mwenye tabia ya aina hiyo, kwenye zizi kuna ng’ombe  na mbuzi pamoja kondoo nitachinja wanyama nipike ndani watoto wale mpaka wakinai.Nitawalea namna hiyo, na ndivyo nilivyofanya kwa upande wa madini.

“Wachimbaji wa wilaya hiyo walikuwa wakivamia Pori la Akiba Kigosi Moyowosi kuchimba madini ya dhahabu kwa njia isiyokuwa rasmi.Rasilimali  hiyo Mungu ameishusha nchini iwanufaishe wananchi hivyo kuliko kuendelea kuiba serikali ikaamua kuwamilikisha.

“Kuliko wapige na askari wa hifadhi, wapelekwe mahakamani, nikasema hapana. Nikamtaka Dk. Doto Biteko na wenzake serikalini waangalie namna watakavyoweza kufanya rasilimali hiyo iwafae vijana wa Bukombe.”

Mgombea Urais Dk.Samia amesema kwa sasa hivi “Wanachimba, wanauza, tumewajengea masoko na maisha yanakwenda vizuri sana. Huku ndiko kujenga utu wa Mtanzania, ndiko kujenga utu wa vijana wetu. Ndiko kuwawezesha waendelee na maisha yao yawe mazuri wapate heshima ya kutosha.”

Pamoja na hayo Dk. Samia ametumia nafasi hiyo kuelezea kuwa katika Bukombe miaka mitatu aliwahakikishia wananchi kwamba atawatumikia kuleta maendeleo na kujenga taifa jumuishi na kazi hiyo Serikali imefanya mambo makubwa katika kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali na kazi hiyo itaendelea.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi hao wa Bukombe ikifika Oktoba 29,2025 wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura kwa wagombea wa Chama hicho ili kazi ya kuleta maendeleo ya wananchi iendelee na kwamba yaliyofanyika katika miaka mitano iliyopita imeonekana na wameweka na katika miaka mitano ijayo wataweza.