Waarabu watia mkono Singida Black Stars

WAKATI Kiungo wa Singida Black Stars raia wa Nigeria, Morice Chukwu akibakisha mkataba wa mwaka mmoja na kikosi hicho, inadaiwa mabosi wa Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia, wako tayari kuipata saini ya nyota huyo katika dirisha dogo.

Taarifa kutoka Tunisia zinaeleza, uongozi wa Esperance chini ya Rais wa timu hiyo, Hamdi Meddeb, unavutiwa na uwezo wa nyota huyo na sasa wanafuatilia upatikanaji wake, kwa lengo tu la kujiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2025.

Kwa mujibu wa mtandao maarufu wa Tunisia wa diwansport.com, Rais wa Esperance, Hamdi anavutiwa sana na uwezo wa kiungo huyo, huku ikielezwa yupo tayari kutoa kiasi cha Sh600 milioni, ili kupata saini yake kabla ya kumaliza mkataba wake.

SING 01

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Singida, aliliambia Mwanaspoti kwa sasa sio muda wa kuzungumzia masuala la usajili kwa sababu dirisha limeshafungwa, kwani malengo yao ni kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki msimu huu.

“Ni mapema sana kuzungumzia suala hilo kwa sasa, ila unajua tangu aje kocha Miguel Gamondi umeona Chukwu alivyo muhimu katika kikosi chetu, kiasi cha kucheza maeneo zaidi ya matatu uwanjani,” amesema kiongozi huyo.

SING 02

Pia, kiongozi huyo amesema mkakati uliopo kwa sasa ni kumuongezea mkataba mpya nyota huyo wa miaka miwili, kwa lengo la kuongeza thamani yake kutokana na kazi anayofanya, hivyo mazungumzo yanaendelea na yapo katika hatua nzuri na menejimenti yake.

Nyota huyo aliyezaliwa Jimbo la Ebonyi, amecheza timu mbalimbali za Tanzania, zikiwamo za Fountain Gate, Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars) na TRA United zamani Tabora United, kisha Go Round FC, Akwa United na Rivers United za kwao Nigeria.