Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekabidhi rasmi kisima cha maji safi na salama katika Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake iliyotolewa mwaka 2023 na sehemu ya juhudi za kurudisha kwa jamii na kuboresha mazingira ya elimu nchini.
Hafla hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya jubilee ya miaka 50 ya shule hiyo na mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba, tukio lililohudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na viongozi mbalimbali wa elimu na serikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, alisema taasisi hiyo itaendelea kuwa mlezi wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo hatua kwa hatua, ikiwa ni sehemu ya jitihada za TCAA za kurejesha kwa jamii.
“TCAA itabaki kuwa mlezi wa shule hii. Tutazidi kushirikiana na uongozi wa shule kutatua changamoto mbalimbali taratibu, ili kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia yanadumu. Maji ni uhai, na tunataka kila mwanafunzi hapa ajifunze katika mazingira safi na salama,” alisema Dkt. Mwinyimvua.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata, Bi. Prisca Barnabas, aliishukuru TCAA kwa mchango huo muhimu na kuahidi kuhakikisha miundombinu ya maji inatunzwa kwa manufaa ya wanafunzi na jamii.
“Tunatoa shukrani za dhati kwa TCAA kwa kujali elimu. Tutahakikisha kisima hiki kinatumika ipasavyo na kudumu kwa muda mrefu,” alisema Bi. Prisca.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Cassian Henry, alisema kisima hicho kitarahisisha upatikanaji wa maji na kuboresha mazingira ya usafi na utunzaji wa bustani za shule.
“Kisima hiki ni msaada mkubwa kwetu. Kitatupa uwezo wa kudumisha usafi, kupunguza gharama, na kufanya shule yetu kuwa mazingira bora ya kujifunzia,” alisema Mwalimu Henry.
Katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, Dkt. Mwinyimvua alipanda mti katika eneo la shule kama ishara ya utunzaji wa mazingira na kumbukumbu ya tukio hilo la kihistoria.
Kisima hicho chenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 20, kinatarajiwa kutatua changamoto ya maji kwa wanafunzi, walimu, na wakazi wa jamii inayozunguka shule hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa kisima cha maji safi kilichojengwa kwa ufadhili wa TCAA kwa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akifungua maji kama ishara ya kukabidhi kisima cha maji safi kilichojengwa kwa ufadhili wa TCAA kwa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Dodoma. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Cassian Henry.
Muonekano wa kisima cha maji safi kilichojengwa kwa ufadhili wa TCAA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akisaini kitabu cha wageni alipowasili Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua akizungumza muda mchache kabla ya kukabidhi kisima
Afisa Elimu Kata, Bi. Prisca Barnabas akizungumza wakati wa mahafali
Picha ya pamoja ya timu ya TCAA
Picha ya pamoja na uongozi wa kata, shule na wadau wa elimu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akipanda mti kama ishara ya kuadhimisha miaka hamsini tangu kuanzishwa kwa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege wakitoa burudani ya ngoma wakati wa hafla hiyo