JUMUIYA ya vijana kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika imeomba kupewa nafasi zaidi kushiriki katika ngazi za maamuzi, hasa katika masuala yanayohusu mabadiliko ya tabia ya nchi.
Wamesema ushiriki wa vijana katika majukwaa ya maamuzi ni hatua muhimu katika kukuza mawazo mapya, ubunifu na kutafuta suluhisho endelevu kuhusu changamoto za mazingira.
“Kupitia nafasi hizo, vijana hujifunza uwajibikaji, huimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, na kuchangia juhudi za kulinda ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.”
Akizungumza na Wanahabari katika mkutano wa kimkakati wa wataalamu wa mabadiliko ya tabia ya nchi, Mkurugenzi wa Asasi za Kiraia Sara Pima amesema changamoto kubwa inayowakabili vijana ni ukosefu wa uwakilishi wa pamoja, kutokana na wengi wao kugawanyika katika makundi mbalimbali badala ya kuwa na sauti moja yenye nguvu katika majukwaa ya maamuzi.
Kwa upande wake, Mshauri wa Rais katika Masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabia ya nchi Dkt. Richard Muyungi amesema vijana ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo ni muhimu wakapewa nafasi kubwa zaidi kushiriki katika kupanga na kutekeleza sera za mazingira ili kulinda mustakabali wao na wa taifa kwa ujumla.
“Vijana ndio tegemezi barani Afrika na vijana hao ndio waathirika wa mabadiliko ya tabia ya nchi na kwa mara ya kwanza Vijana ndio wanapewa fursa katika maamuzi na matarajio yao kwa ajili ya mustakabali wao hautoathiriwa na mabadiliko hayo.”
Nae Muwakilishi kutoka nchi Kenya Abby Chebet amesema Mkutano huo wa Vijana utasaidia kwa nafasi kubwa kubadilishana uzoefu baina ya nchi shiriki.
“Tunategemea mkutano huu utaweza kutusaidia kubadilisha uzoefu binafsi natarajia kujua nchi zingine zina ujuzi n weledi upi kuhakikisha wanatunza Mazingira na Kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.”