Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kupitia upya mchakato wa fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, ili kuhakikisha wanapata haki zao.
Othman maarufu ‘OMO’ amesema hilo litafanikiwa endapo Wazanzibari watamchagua Oktoba 29, akisisitiza kufanya marejeo upya ya utolewaji wa fidia ili haki za wananchi waliopoteza ardhi zao kwa ajili ujenzi huo, kunufaika na mradi huo.
Mgombea huyo, ameeleza hayo leo Jumatatu Oktoba 13,2025 katika mkutano maalumu na wananchi wa Shehia ya Furaha, Wilaya ya Chake Chake, Pemba katika mwendelezo wa kusaka kura kwa awamu ya tatu kisiwani humo, baada ya jana kuihitimisha Mjini Unguja.

Mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo Othman Masoud Othaman akisalimiana Rajab Abdallah, alipowasili Shehia ya Pujini wilayani Chakechake Pemba kuzungumza na wananchi wa Shehia hiyo
Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, amesema kuwa haiwezekani kuona mamia ya watu wanaendelea kudhulumiwa haki zao, hivyo atahakikisha anarejesha tabasamu lao pindi atakaposhika madaraka Oktoba 29.
Katika maelezo yake, Othman ameeleza kuwa kwa nyakati tofauti amekuwa akipokea taarifa za malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu malipo yasiyotimizwa ipasavyo, huku baadhi wakikosa kabisa fidia zao stahiki jambo linalowasababishia umaskini.
“Haiwezekani mtu alikuwa na shamba lake akifanya kilimo kilichokuwa kikimuingizia kipato, leo unakwenda kumpa fedha zisizoendana na uhalisia wa eneo lake. Hii si sawa haikubaliki, siwezi kuvumilia uonevu huu,” amesema Othman.
Othman amesema Serikali atakayoiunda kuanzia Oktoba 29, itahakikisha kila mwananchi aliyepisha mradi huo analipwa fidia yake kwa haki na kwa mujibu wa eneo alilochukuliwa na Serikali.

“Si uungwana na si haki kuchukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya maendeleo halafu mhusika asipate kile anachostahiki. Nitalisimamia hilo, tena kwa ukaribu sana,” ameeleza.
Mmoja wa wananchi waliopisha mradi huo, Abdalla Seif amedai kuwa shamba lake lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya uwanja wa ndege, lakini fidia aliyopewa halingani na thamani ya ardhi yake.
Wakati mkazi mwingine Ali Abdallah Juma amesema eneo lake lililochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba, angeamua kuliuza kwa mtu au watu binafsi angepata Sh100 milioni, lakini fidia aliyoipata haifiki hata Sh50 milioni.
Septemba 25, 2025 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilimkabidhi mkandarasi mradi huo wenye lengo la kuifungua Pemba kiuchumi ili kuanza utekelezaji wake.
Ziara hiyo ya kusaka kura kisiwani Pemba, ilimfikisha OMO hadi Shehia ya Pujini wilayani humo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa Shehia hiyo.