Unguja. Wakati utafiti ukionesha Tanzania na Zanzibar kuwapo na maabara moja inayokidhi vigezo vya kimataifa katika kuhakiki ubora na usalama wa chakula, ukosefu wa sera ya pamoja imetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazochangia tatizo hilo.
Katika utafiti uliofanywa na mradi unaoangalia masuala ya usalama wa chakula na uwezo wa maabara chini ya uratibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya maabara tisa zilizofanyiwa utafiti ni moja ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) iliyokidhi viwango vya kimataifa.
Katika utafiti huo, Tanzania bara zimehusishwa maabara sita na Zanzibar maabara tatu.
Akizungumza katika warsha ya kuhakiki matokeo ya tathmini ya mifumo wa udhibiti wa usalama wa chakula na uwezo wa maabara katika uchunguzi wa usalama wa chakula, leo Oktoba 13, 2025 Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said amesema maabara moja pekee yenye uwezo unaotakiwa.
Amesema changamoto hiyo ni kubwa kwani hata vyeti vinavyotoka vinakuwa havitambuliwi kimataifa jambo ambalo linaharibu ushindani wa bidhaa za Tanzania kwenye masoko ya nje, huku akisisitiza kuwa usalama wa chakula sio suala la kiufundi au kisheria pekee ni suala linalohusu afya ya umma na maendeleo ya Taifa.
“Madhara ya matokeo hayo yasiyoridhisha yamesababishwa na ukweli kuwa Tanzania bara na Zanzibar hazina sera mahususi ya kitaifa ya usalama wa chakula, badala yake zinadhibiti usalama wa chakula kupitia sera na mikakati ya sekta mbalimbali zinazogusa masuala hayo,” amesema.
Amesema sera hizo zinatekelezwa katika ngazi tofauti, changamoto zinazojitokeza ni pamoja na miundombinu isiyotosheleza na kutokuwapo kwa uratibu mzuri wa kazi zinazofanywa na taasisi husika. “Inapotokea taasisi zetu kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi inaweza kuwa na madhara kiafya na kiuchumi.”
“Wakati mwingine unakuta huyu anasema hivi mwingine anasema vile, hii haipo sawa hivyo huu uratibu haupo vizuri na bado kuna ukosefu wa kitaalamu katika tathmini, usimamizi na uchanganuzi wa vihatarishi vya usalama wa chakula,” amesema.
Rashid Suleiman kutoka Chuo cha Kilimo Sua ambaye ni miongoni mwa waliohusika na utafiti huo, amesema kama nchi ni vyema kuanzisha sera ya usalama na miongozo ili kila taasisi na mdau ajue anaingia wapi na majukumu yake na kukuza uwezo katika masuala ya usalama wa chakula.
Mratibu wa Mradi huo kutoka FAO, Diomedes kalisa, amesema mradi huo unafanyika katika nchi za Afrika Mashariki ambao umezinduliwa mwaka jana Septemba na utekelezaji wake umeanza Mei mwaka huu. Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) hadi Desemba 2026.
Lengo ni kujua nchi za Afrika Mashariki zimesimama katika eneo lipi kwenye ubora wa bidhaa zake na mfumo unaoangalia usalama chakula upo katika hali ya namna gani kuhakikisha wanafungua milango ya ufanyaji biashara na nchi zote duniani.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti wa maabara, Kezia Mwambo amesema katika wamefanya ukaguzi katika maabara tisa kati ya hizo sita Tanzania bara na tatu Zanzibar ambapo ni moja ambayo ilionekana ina utambuzi wa kimataifa.
“Ikiwa bidhaa zimepimwa zisiende kupimwa tena kwa sababu tayari zitakuwa zimepata utambuzi kimataifa hivyo itasaidia kuingia sokoni kwa usalama wa chakula kikanda na kimataifa,” amesema
Amesema “Ili bidhaa zikubalike lazima ripoti zinazoambatana na mizigo ziwe zimetoka katika maabara ya kimataifa, na ili maabara zipate lazima zihusike na usimamizi wa ubora nje ya maabara yenyewe yaani ijifananishe na maabara nyingine.”
Amesema nyingine zinashindwa kununua sampuli ya kujifananisha kwa sababu bei kubwa na bado elimu ni ndogo kutengeneza sampuli.
Amesema kuna pengo kutokana na vifaa vya kidijitali watu wanaweza kuamka wakasema bidhaa yetu ina changamoto fulani hivyo kama nchi hatuwezi kujitetea kwa sababu hatuna uwezo wa kupima.”