EALA yaitaka Nelson Mandela kuendeleza tafiti zinazozalisha ajira kwa vijana

Arusha . Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameitaka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) kuwekeza nguvu zaidi katika kufanya tafiti zinazozalisha fursa za kiuchumi na kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana barani Afrika.

Wabunge hao wamesema hayo wakati wa ziara maalumu katika taasisi ya NM-AIST yenye makao yake makuu jijini Arusha.

Akizungumza katika ziara hiyo, mbunge wa EALA na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Elimu ya Juu, Dk Abdullah Makame, amesema Afrika bado ni bara lenye vijana wengi zaidi duniani, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wake wako chini ya umri wa miaka 35, huku wengi wao wakiwa hawana ajira au wako nje ya mfumo wa shughuli za kiuchumi.

“Mnafanya kazi nzuri, hasa kupitia tafiti zinazolenga kusaidia jamii kutatua changamoto. Nawasihi mweke zaidi rasilimali fedha na nguvu katika tafiti zinazozalisha fursa za kiuchumi na ajira endelevu kwa vijana, kwani ukosefu wa ajira bado ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazokabili nchi zetu za bara la Afrika,” amesema Dk Makame.

Makame amesema hayo wakati taarifa za Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zikionyesha kuwa Afrika kwa sasa ina zaidi ya vijana milioni 420 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 35, idadi inayotarajiwa kuzidi milioni 830 ifikapo mwaka 2050.

Aidha kati ya hao,  theluthi moja hawana ajira na wamekata tamaa ya kupata ajira huku theluthi nyingine wanashiriki katika kazi zisizo rasmi na hatarishi, na mmoja kati ya sita tu ndio wameajiriwa rasmi.

Aidha inaonyesha kuwa kila mwaka, kati ya vijana milioni 10 hadi 12 wanaingia mitaani kusaka ajira huku  zinazozalishwa takribani milioni 3.1 pekee na kuacha zaidi ya asilimia 69 bila ajira na kusababisha ukosefu wa utulivu wa kijamii na kiuchumi.

Dk Gabriel Garang Aher, mbunge wa EALA anayewakilisha Sudan Kusini, amesema upo umuhimu wa kuingiza teknolojia na akili bandia (AI) katika tafiti ili kuwawezesha vijana kuunda ubunifu na kujiajiri wao wenyewe pamoja na wengine.

“Ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo sugu ambalo limechochea migogoro na machafuko katika nchi nyingi. Kuna hitaji la dharura la kuunda fursa mpya kwa vijana kupitia tafiti zinazotumika na ubunifu unaoweza kutoa suluhisho endelevu kwa tatizo hili.”

Naye David Ole Sankok, akiwakilisha Zanzibar, amesema kuwa ikiwa idadi kubwa ya vijana wa Afrika itatumika ipasavyo, inaweza kuwa nguvu kubwa ya kuendesha uzalishaji, ukuaji jumuishi, na maendeleo endelevu barani Afrika.

Ametumia fursa hiyo kuitaka NM-AIST kuhakikisha mpango wake wa tafiti unajumuisha jamii za asili, ambapo maarifa na desturi zao huchangia kwa maana katika maendeleo endelevu.

Sankok pia aliitaka taasisi hiyo kuanzisha mikakati bunifu ya kuunga mkono biashara za mipakani, kusaidia wafanyabiashara wadogo kuongeza thamani ya bidhaa zao na kushindana vyema katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa taasisi hiyo anayeshughulikia masuala ya kitaaluma, utafiti na ubunifu wa NM-AIST, Profesa Anthony Mshandete, amesema taasisi hiyo ni sehemu ya mtandao wa Pan-Afrika wa vyuo vya sayansi na teknolojia ulioenea sehemu mbalimbali za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Taasisi hizi, zilizoongozwa na maono ya marehemu Nelson Mandela, zimeundwa kuandaa na kukuza kizazi kijacho cha wanasayansi na wahandisi wa Kiafrika wanaoweza kuendesha mabadiliko ya bara letu kupitia sayansi, uhandisi, teknolojia na ubunifu (SETI),” amesema.

Ameongeza kuwa jukumu kuu la NM-AIST ni kutoa tafiti na ubunifu unaokabiliana moja kwa moja na changamoto za jamii.

“Kuwa na wabunge wa EALA hapa, ambao wanawakilisha wananchi zaidi ya milioni 300, ni fursa kubwa ya ushirikiano, hasa katika kulinganisha kazi zetu na vipaumbele walivyoleta,” amesema.

“Sisi tunashukuru sana na tunaahidi kufanyia kazi yale yote waliyotuomba kusaidia ili kunusuru kizazi kijacho kiuchumi.”

Mshandete amesema kwa sasa wanapanga kuandaa mdahalo wa wadau kutoka sekta za elimu, utafiti, biashara na sera ili kujadili mikakati thabiti ya utekelezaji wa mapendekezo ya wabunge hao kwa ufanisi na matokeo yanayoonekana.