Aman Josiah kutua Dodoma Jiji

DODOMA Jiji ipo hatua za mwisho kumchukua kocha Aman Josiah ili kuziba pengo la Vincent Mashami raia wa Rwanda wanayetaka kuachana naye ikitajwa sababu ya kukosa vigezo vya kukaa benchi kama kocha mkuu.

Oktoba 3, 2025, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilitoa adhabu kwa Dodoma Jiji kulipa Sh15 milioni kutokana na kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara bila ya kuwa na kocha mkuu mwenye sifa kwa mujibu wa kanuni ya 77:3 (1,2,3).

Dodoma Jiji ambayo ilimtambulisha Mashami kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho akichukua nafasi ya Mecky Maxime, imeshindwa kumtumia Mnyarwanda huyo kutokana na kukosa vigezo vinavyotakiwa kikanuni ambapo kocha wa kigeni anapaswa kuwa na leseni ya Uefa Pro.

Chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti kwamba: “Leseni yake hajaifanyia maboresho (Refresher), tulitarajia angefanya hivyo ili kwa bahati mbaya mambo hayakwenda kama tulivyotarajia hivyo tupo hatua ya mwisho ya kumalizana na Josiah ili aje kuziba pengo lake.”

AMA 01

Alipotafutwa Josiah aliyeisaidia Tanzania Prisons kutoshuka daraja msimu uliopita amesema: “Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote ila kuna timu nyingi zimeleta ofa, nitakayomalizana nayo basi nitakuwa tayari kuzungumza.”

Kwa kipindi ambacho Josiah alikaa nje ya kazi baada ya kuachana na Tanzania Prisons msimu wa 2024-2025 ulipomalizika alikuwa anasoma na sasa ana Diploma A ya CAF inayomfanya kuwa na vigezo vya kusimama kwenye benchi la timu yoyote ya Ligi Kuu Bara akiwa kocha mkuu.