Staa Simba apigilia msumari, amchomoa Camara kikosini

MOUSSA Camara ndiye kipa namba moja wa kikosi cha Simba ambapo kiwango alichokionyesha kwenye Ligi Kuu Bara 2024-2025 ukiwa ni wa kwanza kwake, anawekwa levo moja na Djigui Diarra wa Yanga kufuatia msimu uliopita kufukuzana kwa ukaribu kwenye clean sheet. Hata hivyo, aliyewahi kuwa beki wa Simba, Salim Mbonde, amemtaja Diarra kuwa namba moja mbele ya Camara.

Mbonde ambaye pia amewahi kuizitumikia JKT Oljoro, Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ametaja sababu za kumchomoa Camara na kumuweka Diarra kuwa namba moja.

Mbonde amesema ubora aliouonyesha Diarra tangu amekuja Tanzania anastahili kuwa namba moja katika kikosi chake.

Mbali na Diarra, lakini Mbonde ambaye ameamua kustaafu kucheza mpira wa miguu kutokana na kusumbuliwa na majeraha, amelia na mchezaji namba tisa bora akisema hakuna wa kiwango kikubwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, beki huyo amesema amekuwa akifuatilia Ligi Kuu Bara ambapo alipotakiwa kutaja kikosi chake bora kwa sasa, alianza na Diarra golini, huku pia baadhi ya mastaa wengine akiwapiga chini akiwamo Pacome Zouzoua.

CAMA 01

Katika kikosi hicho aliwataja nyota sita wa Yanga, Azam (3) na Simba (2). Kikosi kipo hivi; Djigui Diarra, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ’Tshabalala’, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Himid Mao, Idd Seleman ‘Nado’, Mudathir Yahya, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Clement Mzize.

“Kwa sasa wachezaji wengi wanafanya vizuri na nimekuwa nikiwafuatilia, Diarra hana mpinzani ni kipa bora anastahili kukaa hapo, Kapombe bado anacheza kwa ubora, Tshabalala pia kila mmoja anaona Bacca na Job wameshatengeneza ufalme wao kuanzia Yanga hadi Stars.

CAMA 02

“Kwa upande wa Himid nampa nafasi hiyo kutokana na kucheza kwa mafanikio misimu zaidi ya mitano nje ya nchi lakini pia amerudi na anapata namba Azam, Nado anakuwa bora siku hadi siku, tunamuona hata timu ya taifa anachofanya, Mudathir namba zinapanda Feisal pia anacheza kwa ubora mkubwa,” amesema.

Anasema eneo la namba tisa amepata ukakasi kidogo hakuna wafungaji bora tofauti na miaka ya nyuma lakini ameona ubora kidogo kwa Gomez ndio maana amempanga huku akimtaja Mzize kuwa ameimarika na anazidi kuwa bora anastahili kuwa mchezahi wa mwisho kwenye kikosi chake.

CAMA 03

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha Diarra ambaye huu ni msimu wa tano kucheza Ligi Kuu Bara akiitumikia Yanga, amejenga ngome yake kikosini hapo sambamba na timu ya taifa ya Mali.

Katika misimu miwili ya mwanzo akiwa Yanga 2021-2022 alimaliza na clean sheet 15 na 2022-2023 clean sheet 17, akatwaa Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara, kisha akaendelea kuwa namba mbili 2023-2024 nyuma ya Ley Matampi aliyekuwa Coastal Union kufuatia kumaliza na clean sheet 14, mwenzake akiwa na 15.

Msimu uliopita 2024-2025, bado washindi wa tuzo hawajatangazwa, lakini Camara amemaliza kinara wa clean sheet 19, Diarra akiwa na 17.

Mbali na hapo, Diarra huu ukiwa ni misimu wa tano ndani ya Yanga, tayari ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii (4), Kombe la FA (4), pia akiifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023.

Msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara, Diarra amedaka katika mechi tano za mashindano akiwa hajaruhusu bao hivyo amekusanya clean sheet tano, huku Camara mechi nne, ameruhusu mabao mawili akiambulia clean sheet mbili.

Mbonde aliongeza kwamba, anaona Diarra hana maisha marefu ndani ya kikosi cha Yanga kwani ubora wake unazifanya timu mbalimbali kumpigia hesabu za kumsajili kama ilivyotokea kwa Stephane Aziz Ki.

“Diarra ubora wake anaoendelea kuuonyesha msimu hadi msimu sioni akiendelea kukaa Ligi Kuu Bara, muda si mrefu ataondoka na kwenda kushindana na makipa wengine bora kama kipa wa Mamelodi, hii ni kutokana na aina yake ya uchezaji wa kisasa.

“Hata ikitokea akaondoka kama ambavyo naamini kuwa atafanya hivyo, atakuwa ameacha alama kubwa kwenye ligi yetu kwani tayari vijana hasa wa kikosi ambacho nafundisha mimi huwa na matamanio ya kuwa bora kama kipa hiyo kwa kuanzisha mashambulizi kutoka chini,” amesema.

Mbonde alisema Diarra ni kipa wa kisasa na amefanya hivyo kwa vitendo wachezaji wengi wanavutiwa na aina yake ya uchezaji akiweka wazi kuwa tayari amekutana na makipa wengi vijana ambao wanatamani kuwa na uchezaji wa aina yake.

“Uwanja wa mazoezi makipa wanaelekezana uwanjani na mabeki wao kuwa waanzishiane mipira kutoka nyuma kama anavyofanya Diarra, hii tayari ni alama kubwa inabaki kwa vizazi vijavyo, hivyo hata akiondoka kutakuwa na kina Diarra wa ndani,” amesema.

Akimuelezea zaidi Diarra, Mbonde alisema kipa huyo ni habari nyingine kwenye Ligi ya Tanzania kwani ukiondoa ushindani wa ndani amekuwa kipa namba moja wa timu yake ya taifa ya Mali ambayo imekuwa ikimuamini kwenye mashindano yote makubwa na madogo.

Amesema Diarra ni kipa ambaye anajiamini na ana uwezo mkubwa wa kucheza na miguu.