BEKI wa kushoto wa Yanga, Mohamed Hussein Zimbwe Jr ametuma salamu mpya kwa wale wote wanaosema hana furaha tangu ajiunge na kikosi hicho.
Zimbwe aliyetua Yanga katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu baada ya kumaliza mkataba ndani ya kikosi cha Simba, alisema anashangazwa na habari hizo, kwani vitu vyote ambavyo huwa anavifanya katika maisha yake anakuwa na malengo anayojiwekea na pale anapoyati-miza huwa anajisikia furaha.
“Hizi habari watu wanazitoa wapi kuwa mimi sina furaha na timu niliyopo? Wao wamekuja? Ni habari mbaya sana na za uchonganishi, mimi naziona tu huko mitandaoni, kwanza kwa nini watu wanisemee kuwa sina furaha? Sasa niwaambie tu kila mtu angependa kuwa mwenye furaha kwa sehemu aliyopo, hivyo mimi nina furaha kama zote kwa mahali nilipo,” amesema Zimbwe baada ya mashabiki mtandaoni kusema amehamia Yanga, lakini hana furaha ma kwamba amepoteza namba mbele ya Chadrack Boka wakati ndani ya Simba alikuwa panga pangua.

“Unajua lengo mojawapo la mwanadamu katika maisha yake hapa duniani ni kuitafuta furaha, kwamba purukushani zote hizi katika maisha zina lengo la kuisaka furaha, kila mtu anapenda kuwa na furaha kwenye maisha yake, vyote tunavyovifanya na malengo tunayoweka na pale tunapoyatimiza huwa tunajisikia furaha, watu waache uzushi wao na wasiwe wasemeji wangu,” amesema Zimbwe Jr.
Hivi karibuni kumezuka mijadala katika mitandao ya kijamii kuwa tangu Zimbwe Jr alipojiunga na Yanga SC, wakidai hana furaha ndani ya timu hiyo kongwe na mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.
Zimbwe kutua kwake Yanga msimu huu, kulihitimisha takribani miaka 11 aliyohudumu ndani ya Simba aliyojiunga nayo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.
Katika kipindi cha miaka 11 akiwa Simba, Zimbwe amekuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya kikosi hicho kwa kushinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Pia ameshinda makombe ya FA na Ngao ya Jamii.

Zimbwe pia amechangia Simba kufanya vizuri katika michuano ya CAF, huku timu hiyo ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita 2024-25 na kupoteza mbele ya RS Ber-kane. Kabla ya hapo, imeishia robo fainali za CAF mara tano kuanzia 2018.
Msimu huu baada ya kutua Yanga, Zimbwe ameanza na ubingwa wa Ngao ya Jamii, baada ya kuifunga Simba bao 1-0, huku kikosi hicho kikiwa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ku-wania kufuzu makundi.

Upande mwingine, Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, amesema kwa asilimia kubwa maan-dalizi ya kikosi hicho kuelekea mechi ya hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi yanakwenda vizuri, huku akipata tabasamu kufuatia kupewa taarifa za mastaa wake wengi waliokwenda timu zao za taifa kuwahi kambini.
Alhamisi ya Oktoba 16, 2025, Yanga itaanza safari ya kwenda Malawi kwa ajili ya mechi hiyo ambayo Folz amepania kurudi Dar na ushindi kama ilivyokuwa hatua ya awali dhidi ya Wiliete SC ya Angola.
Akizungumza na Mwanaspoti, Folz amesema, Yanga ina kikosi kipana, hivyo hana hofu kwani licha ya mastaa kuwa kwenye majukumu ya kimataifa lakini bado ana uhakika wa kufanya vi-zuri dhidi ya Silver Strikers huku akibainisha kwamba mabosi wa klabu hiyo tayari wameshampa uhakika kwamba wachezaji wote watakuwa wamesharejea kabla ya mechi hiyo ya ugenini.
“Tangu nianze kuifundisha Yanga, kumekuwa na mapumziko haya ya timu za taifa, lakini bado haijazuia ubora wa kikosi changu kupata matokeo mazuri.
“Mpaka sasa nina uhakika ya kwamba tutakuwa na wachezaji wote walioko kwenye timu za taifa, kwani watakuwa wamesharejea, hivyo niwatoe shaka mashabiki wanaodhani tutawakosa baadhi ya wachezaji,” amesema Folz.
Alisema bado hajawasoma Silver Strikers kwa upana sana, lakini hata iweje anachotaka ni ushindi uanzie ugenini mpaka nyumbani.
“Wapinzani tutawaheshimu tu ila kiukweli kabisa tutakwenda kucheza soka la kushambulia ili kujihakikishia tunapata ushindi kuanzia ugenini hadi nyumbani.
“Yanga ina kikosi kipana sana na chenye wachezaji wakubwa, hivyo mpinzani anatakiwa ku-tuogopa sisi, ila ni kosa kwetu kumuhofia adui yetu.
“Nimeshawaona wachezaji waliokuwa mazoezini na hata waliokuwa katika timu za taifa, wote wako timamu na tayari kwa mechi hiyo muhimu,” amesema Folz.
Tangu Yanga ianze mazoezi Oktoba 6, 2025 kuelekea mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi ya Oktoba 18, 2025 nchini Malawi, mastaa waliokosekana kambini kutokana na majukumu ya timu zao za taifa ni Duke Abuya (Kenya), Pacome Zouzoua (Ivory Coast), Prince Dube (Zimbabwe), Celestin Ecua na Lassine Kouma (wote Chad). Pia Israel Mwenda, Ibrahim Bacca, Offen Chikola na Bakari Mwamnyeto wanaocheza kikosi cha Tanzania. Pia Dickson Job na Aziz Andabwile walikuwa na kikosi cha Tanzania, kabla ya kurejea kambini Yanga baada ya mechi ya kwanza ya Zambia iliyochezwa Oktoba 8, 2025.
Ecua na Kouma, tayari wamemaliza majukumu yao ya kuitumikia Chad tangu jana Jumapili Oktoba 12, 2025, hivyo wanawahi kurudi kama ilivyo kwa Dube anayemaliza majukumu yake leo Jumatatu Oktoba 13, 2025. Kwa upande wa nyota wanaocheza timu ya taifa ya Tanzania, wanamaliza majukumu yao kesho Jumanne Oktoba 14, 2025 kwa kucheza dhidi ya Iran huko Dubai, kisha Jumatano Oktoba 15, 2025 saa 4 asubuhi wanatarajiwa kurudi Dar.
Taarifa zilizopo ni kwamba, Pacome na Duke abuya ambao timu zao zinakutana kesho Jumanne Oktoba 14, 2025 saa 4 usiku, wanatarajiwa kuungana na wenzao nchini Malawi.