Waandishi waeleza mikakati ya kutumia mafunzo ya UTPC

Iringa. Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wameeleza dhamira yao ya kutumia mafunzo waliyopata kupitia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa kushirikiana na International Media Support (IMS), kuboresha ubora wa kazi zao kwa kuandika habari zenye tija zinazogusa maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Waandishi hao wametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Oktoba 13, 2025, walipozungumza na Mwananchi kuhusu mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Lumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Wamesema yamewapa dira mpya ya kitaaluma na ari ya kutumia kalamu zao kama chombo cha kuibua changamoto, kuhamasisha uwajibikaji na kuhimiza mabadiliko chanya kwenye jamii.

Mwandishi wa Gazeti la Nipashe kutoka mkoani Iringa, Flora Kamaghe amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa wajibu wa mwandishi katika kuandika habari zenye suluhisho kwa watu.

‎Waandishi wa habari mikoa ya nyanda za juu kusini wakiwa katika ukumbi wa mikutano uliopo hoteli ya Lumilo halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakijadili mikakati ya kutumia mafunzo  waliyopata kupitia  Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na International Media Support (IMS) ili kuboresha ubora wa kazi zao kwa kuandika habari zenye tija, zinazogusa maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo katika jamii.

“Tumejifunza kuandika habari zenye majibu kwa jamii, zinazochochea mabadiliko na tutatumia kalamu zetu kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika na changamoto zao zinapata ufumbuzi,” amesema Kamaghe.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Hakimu Mwafongo amesema mafunzo hayo yamewakumbusha wanahabari umuhimu wa kutumia taaluma yao kutenda haki kwa jamii.

“Tuitendee haki jamii. Kalamu zetu ziwe chombo cha kuibua changamoto na kufuatilia utekelezaji wa sera, si kwa upendeleo au kwa maslahi binafsi,” amesema Mwafongo.

Mdau wa habari kutoka Iringa, Raphael Mtitu amesema mafunzo hayo yamempa uelewa wa namna ya kuandika habari zenye matokeo chanya na zinazochangia kuleta suluhu katika jamii.

“Tunatarajia kuona mabadiliko kwenye maudhui ya habari. Ziandikwe kwa lengo la kusukuma maendeleo, si kwa kupendezesha macho ya watu, huo ndio uzalendo wa kweli,” amesema Mtitu.

Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dastan Kamanzi amesema TMF inataka kuona mageuzi makubwa ya namna wanahabari wanavyoandika, ili tasnia ya habari iwe chombo cha kuibua changamoto na kuhoji uwajibikaji wa viongozi wa umma na taasisi binafsi.

“Tunahitaji uandishi unaogusa maisha ya watu na kuchochea uwajibikaji. Huu ndio uandishi unaojenga taifa lenye maendeleo na uwazi,” amesema Kamanzi.

Ameongeza kuwa TMF itaendelea kushirikiana na wadau wengine kuboresha ubora wa habari kupitia mafunzo, ruzuku za miradi ya habari na ufuatiliaji wa matokeo ya kazi za waandishi wanaonufaika na programu hizo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Frank Leonard amewataka waandishi kuacha tabia ya uandishi wa kusifia na badala yake kusimamia misingi ya taaluma, kuuliza maswali magumu na kuandika kwa maslahi ya umma.

“Kuna wimbi jipya la waandishi wanaoandika kwa upendeleo au maslahi binafsi, ila tunapaswa kurejea kwenye misingi ya taaluma yetu na kusimamia ukweli bila woga,” alisema Leonard.

Naye Victor Maleko kutoka UTPC, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaunganisha waandishi na jamii wanayoihudumia, ili maudhui wanayozalisha, yazingatie mahitaji halisi ya wananchi.

“Tunataka habari zenye uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya watu. Kupitia mafunzo haya, waandishi wamepata uelewa wa namna ya kuandika habari zenye athari chanya kwa jamii,” amesema Maleko.

Mafunzo hayo ni sehemu ya programu endelevu za UTPC na IMS zinazotekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini, zikiwa na lengo la kuimarisha ubora wa vyombo vya habari, kukuza uandishi wa uwajibikaji na kuimarisha imani ya jamii kwa wanahabari.