Mbeya. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Ismail Ussi amesema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maji ni sehemu ya ndoto ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wa mijini na vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.
Ussi ameyasema hayo leo, Jumatatu Oktoba 13, 2025, wakati akikagua ujenzi wa tangi la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano kwa siku kutoka chanzo cha Mto Kiwira wilayani Rungwe, mkoani Mbeya ambacho kitawahudumia watu milioni 1.4. Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh119 bilioni.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025,Ismail Ussi akitoka kukagua utekelezaji wa mradi wa tanki la maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya. Picha na Hawa Mathias
“Miongoni mwa mambo ambayo mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, alitamani kuyafanya ni pamoja na kuboresha miundombinu ya maji mijini na vijijini sambamba na kusikiliza kero za wananchi na kuunda wizara maalumu ya kusimamia sekta hiyo,” amesema Ussi.
Amebainisha kuwa Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo ule wa chanzo cha maji kutoka Mto Kiwira unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Mbeya (Mbeya-Uwsa).
“Rais anaendeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru kwa vitendo kwa kuja na kampeni ya maji inayolenga kuwatua wanawake ndoo kichwani na kujenga imani kubwa kwa wananchi,” ameongeza.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu, Ismail Ussi akisalimiana na Mgombea Ubunge Uyole Dk Tulia Ackson, aliposhiriki ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa tenki la maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya. Picha na Hawa Mathias.
Amesema katika halmashauri zote 195 ambazo Mwenge wa Uhuru umepita mwaka huu, hakuna hata moja isiyokuwa na miundombinu ya maji safi na salama.
Katika hatua nyingine, Ussi amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo na kulinda amani na utulivu wa nchi.
Aidha, amesisitiza wananchi kuendelea kuisemea vyema Serikali na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ili ikamilike kwa wakati.
Akizungumza katika mapokezi hayo ya Mwenge, Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mbeya-Uwsa), Mhandisi Barnabas Konga, amesema mradi huo wenye thamani ya Sh119 bilioni, utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika mikoa ya Mbeya na Songwe.

Amesema kukamilika kwake kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 76 hadi kufikia lita milioni 193 kwa siku na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali hiyo unafikia lita milioni 1.4 kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
“Huduma ya maji itaongezeka kutoka saa 21 hadi saa 24 kwa siku hatua itakayochochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi,” amesema Mhandisi Konga.
Ameongeza kuwa hadi kufikia Agosti 2025, Serikali kupitia Wizara ya Maji ilikuwa imeshatoa Sh23 bilioni kati ya Sh26.7 bilioni zinazodaiwa na mkandarasi mshauri na mhandisi wa mradi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole, Dk Tulia Ackson amesema mradi huo utakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Mbeya Mjini na Uyole.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa nikiwa mbunge wa Mbeya Mjini, na sasa ninagombea Uyole. Tutahakikisha tunausimamia kwa karibu hadi ukamilike kwa ufanisi,” amesema Dk Tulia.
Mkazi wa Mtaa wa Forest Jiji la Mbeya, Fausta Noel amesema wanatarajia kukamilika kwa mradi huo kutawaondolea changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi, huku akipongeza Serikali kwa hatua ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa vitendo.