Simulizi ya usafiri wa mwendokasi Mbagala ikiwa ni siku ya pili

Dar es Salaam. Wakati usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) kwenye njia ya Mbagala ikiingia siku ya pili leo Oktoba 13, 2025, baadhi ya abiria wameeleza uzoefu wao katika usafiri huo kwenye njia hiyo.

Miongoni mwa karaha walizozitaja ni foleni isiyokwisha kwenye dirisha la kununua kadi na kulipia kadi hata hivyo wamepongeza huduma inayotolewa, ikiwamo kuelekezwa na wahudumu kwenye kila hatua na kutosubiri basi kwa muda mrefu.

Katika kupishana kati ya basi moja na jingine, Mwananchi imeshuhudia kwenye kituo cha Gerezani, basi A likitoka saa 6:45 mchana na lililofuatia likitoka saa 7:04 mchana na kufika mwisho wa safari Mbagala  kwenye kituo cha BRT Complex saa 1:49 mchana.

Mmoja wa madereva ambaye aliomba hifadhi ya jina kwa kuwa si msemaji wa Mofat, kampuni inayotoa huduma ya usafiri kwenye njia hiyo, alisema utaratibu waliopewa ni kila baada ya dakika tano hadi 20 kutegemea na idadi ya abiria  gari inatoka.

“Kikubwa unachotakiwa ni kutoa gari ikiwa levo siti,” amesema akihesabu siti za moja ya magari hayo na kupata viti 41.

“Unaweza kuiondoa ikiwa pungufu ya abiria watatu au wanne si mbaya,” amesema huku Mwananchi ikimshuhudia pia akielekezwa na kiongozi wake kusafiri na vijana wengine wawili ambao ni madereva ili kuwaelekeza.

Usafiri wa mwendokasi kwenye njia ya Mbagala ambao ulianza majaribio Oktoba 10 na 11 kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali,  Gerson Msigwa na jana Jumapili Oktoba 12,2025  ndipo ulianza kubeba abiria.

Msigwa aliiambia Mwananchi jana Oktoba12, 2025 kwamba majaribio yalianza Ijumaa iliyopita na Jumamosi bila abiria na jana Jumapili mabasi hayo yalianza kupakia abiria.

Leo Jumatatu imeshuhudia abiria wachache wakiwa na kadi za kielektroniki ambazo ndizo zinatumika kwenye usafiri huo, baadhi wakichanja (kuswipe) mara mbilimbili kwa kutokujua na kujikuta wakipata hasara.

Mbali na ugeni wa kadi, pia kwenye dirisha zinakouzwa kadi hizo na lile la kuongeza salio, foleni ni kubwa na haitembei hususani katika kituo cha Gerezani na kile cha Rangitatu (Mbagala) abiria wakisubiri kwa muda mrefu na wengine kukata tamaa na kuondoka.

Abiria wengi walionekana kulalamikia foleni hizo, huku baadhi ya wahudumu wakiwashauri pia wale wenye simu janja kuzitumia kukata tiketi ili kuepuka usumbufu wa foleni ambayo abiri mmoja alitumia takribani dakika tano hadi 10, kupata kadi au kuongeza salio kwenye kadi katika vituo vya

Tofauti na huduma wanayotoa wahudumu wa njia ya Kimara Gerezani, njia ya Gerezani Mbagala kati ya saa 5 asubuhi hadi saa 8:39 mchana wa leo Oktoba 13, 2025 wahudumu wa mabasi hayo ndani ya vituo walionekana kuwa wengi kuliko abiria huku mara zote wakitoa msaada wa kuelekeza abiria.

Kwenye kituo cha Gerezani, Mwananchi ilishuhudia kwenye lango kuu la kuingilia wahudumu wakiwa zaidi ya watano wakiwasaidia na kuwaelekeza abiria namna ya kuswipe kadi zao.

Baada ya hatua hiyo, mbele kidogo kama mita 10, walikuwepo wahudumu wengine wawili wakiwaelekeza abiria namna ya kuvuka kwa usalama kwenye pundamilia ili kupanda basi na kwenye ngazi za kuelekea kupanda basi walikuwepo wengine wawili wakikaribisha abiria.

“Hii ni kwa sababu ni mpya, ngoja tuwape mwaka mmoja huduma hizi hatutaziona,” amesema mmoja wa abiria huku wahudumu hao wakitabasamu na kudai hiyo ni huduma endelevu.

Baada ya dakika takribani 15 za kusubiri, basi lilifika na abiria kupanda na ndani ya basi alipita mhudumu mwingine na kutangaza basi hilo kuanza safari ndani ya dakika mbili, likiwa levo siti.

Vilevile Mwananchi imeshuhudia katika kituo cha Gerezani upande abiria wa Mbagala wanakopandia kukiwa na gari la Polisi wa kutuliza ghasia ambao mara kadhaa walikuwa wakifanya doria ,kabla ya kuwaachia askari wa kampuni ya ulinzi.

Baadhi ya abiria wamekuwa na sintofahamu kama huduma wanayoipata hivi sasa katika mabasi hayo kwenye njia ya Mbagala itakuwa endelevu au ni kwa sababu ya upya?.

Stephano Muso amesema huduma katika mabasi hayo kwenye njia ya Mbagala hajawahi kuiona tangu usafiri huo uanze.

“Sijui labda kwa kuwa hii ni kampuni binafsi na wale wa kwanza (barabara ya Morogoro) ni Serikali!! Hawa (Mofat) kila sehemu abiria ukifika unaelekeza, ngoja wamalize mwaka tuone,” amesema.

Abiria mwingine, Regina Elius amesema kwa jana na leo wafanyakazi  ni wengi kuliko abiria.

“Wanatoa huduma nzuri, hatujui huenda ni sababu ya upya, wacha tuone huko mbele itakuwaje?,” amesema.

Husna Husein yeye kilio chake ni vibanda vya kukatia tiketi na kununulia kadi kuwa vichache.

“Muda huu ni mchana saa 7, abiria si wengi lakini foleni ni kubwa, asubuhi na jioni nini kitatokea? Matokeo yake unapunguza foleni ya kupanda basi, lakini kwenye kulipia kadi foleni inashamiri, waliangalie hilo,” amesema.