Unguja. Dola za Marekani 43 milioni (zaidi ya Sh105 bilioni) zitatumika katika mradi wa ujenzi, upanuzi na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja Zanzibar huku vikitajwa vikwazo vilivyojitokeza mpaka kufikia hatua hiyo.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 Ikulu, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hatua hiyo ni muhimu kwani wamekutana na vikwazo vingi mpaka kufikia hatua hiyo hivyo ni historia imesndikwa.
Amesema safari ya kuanza mipango ya kujenga na kukarabati hospitali hiyo ilianza muda mrefu lakini ilikumbana na vikwazo kutokana na mradi huo kuwa na wafadhili watatu tofauti hivyo kila walichokuwa wakipanga wanashindwa kukubaliana.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Badea na Mfuko wa Maendeleo wa Soudiarabia na Queit.
“Mradi huu umekutwa na vikwazo vingi, tulifika wakati tukaanza kukata tamaa, Namimi niliwaambia wenzangu kwamba hii tufanye marekebisho ya mwisho ikishindikana tutaangalia namna ya kutumia fedha zetu za ndani, nashukuru niliposema hivyo na ndio ikawa hatua ya mwisho mambo yakakamilika,” amesema
Amesema baada ya kukamilika mradi huo watatafuta wataalamu wa uendeshaji wa hospitali hiyo kisasa ili zile huduma zote ambazo zilikuwa zikifuatwa Tanzania bara na nje ya Nchi zipatikane hapo kwa uendelevu.
Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na magonjwa ya moyo, Ubongo na uti wa mgongo ambavyo vitafanyika Zanzibar ikizingatiwa kwa sasa huduma hizo zinatolewa nje ya nchi.
Amesema itaboresha huduma za kibingwa
Dk Mwinyi amesema wakati anaingia madarakani aliahidi kuboresha huduma za afya, akitaja sababu mbili zilizomsukuma ikiwa ni: kuwasaidia wananchi wawe na afya nzuri kwani bila afya hata maendeleo hayawezi kuja.
“Kubwa Zaidi mimi ni mtaalamu wa afya, sasa kushindwa kuboresha huduma za afya ni kushindwa pakubwa bora nishindwe katika sekta zingine, ninafuraha kusema kwamba tumepiga hatua kubwa katika sekta ya afya na hapa ni mwanzo tutaifanya makubwa zaidi,” amesema.
Ameiagiza Wizara ya Afya kuisimamia kampuni inayojenga mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mngereza Mzee Miraji alisema Hospitali ya Mnazimmoja imekuwa nguzo muhimu ya utoaji huduma za afya hivyo kuchelewa kwake ilikuwa ni kuathiri malengo ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya.
Amesema ujenzi wa mradi huo unaenda sambamba na maboresho ya hispitali ya Wazazi ya Mwembeladu na Kidongochekundu.
Kwa mujibu wa Dk Mngereza kwasasa Hospitali ya Mnazimmoja inavitanda 776 na baada ya maboresho hayo itakuwa na vitanda 952.
“Hospitali hii sasa itakidhi viwango vya kimataifa vya kutoa huduma za afya, baada ya kukamilika itaondosha hata mrundikano wa wagonjwa wengi watakuwa wakija na kurudi,” amesema
Pia kutakuwa na vyumba maalumu vya kitabibu vya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, damu, huduma ambazo kwasasa hazitolewi katika Hospitali hiyo licha ya kuwa ya Rufaa.
Pia amesema vitaongezeka vitanda vya wagonjwa mahututi na upasuaji kufikia vitanda 16 kutoka vitanda 13 vilivyopo Sasa ambavyo hatahivyo havina viwango vya kimataifa.
Katika upande wa hospitali ya Mwembeladu, kwasasa ina ghorofa mbili lakini baada ya ukarabati huo itakuwa na ghorofa nne.
Naye Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui amesema haikuwa kazi rahisi kufikia hatua hiyo kwani wamekuta mpango huo upo lakini ulikuwa unakwama.
“Mradi huu ni muhimu kwa Zanzibar, lakini ulikuwa na ugumu wake, sio kazi rahisi wafadhili watatu mpaka wakubaliane, lakini tumefanikiwa,” amesema.
Amesema Dk Mwinyi amejizatiti kuleta mabadiliko makubwa ya afya na kwa maelekezo yake wamefanikiwa kuimarisha huduma katika sekta hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni inayotekeleza mradi huo, Prosper August amesema wamefarijika kuona wanaaminiwa kutekeleza mradi huo na watalinda Imani hiyo kwa kuzingatia mkataba na kutekeleza mradi huo kwa viwango
“Tunajizatiti kutekeleza mradi huu kwa viwango kwa mujibu wa mkataba na ufansii wa hali ya juu,” amesema August.
Utiaji saini kati ya Wizara ya Afya na kampuni ya ujenzi ya China Jiangxi International Economic and Technical Cooparation CO, JV China IPPR International Engineering Co