Mbeya. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuboresha mifumo ya kukabiliana na majanga na maafa, sambamba na mabadiliko ya tabianchi.
Amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika juhudi hizo.
Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 13, 2025, mkoani Mbeya wakati akitoa tamko katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa Duniani.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga mbalimbali.
Katika tamko hilo, Waziri Mkuu amewataka wadau wa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kukabiliana na majanga, sambamba na wananchi kutumia taarifa za tahadhari pindi zinapotolewa.
“Tunampongeza Rais, Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kimkakati katika kuimarisha mifumo ya maafa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, tunasisitiza kuendelea kwa ushirikiano huo,” amesema Majaliwa.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yametokana na Azimio Na. 14/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa Desemba 21, 2009, likiwa na lengo la kukuza utamaduni wa usimamizi na maandalizi ya kurejesha hali baada ya maafa.
Amesema maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kujenga ustahimilivu na ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kupunguza athari za maafa nchini na duniani kote.
Majaliwa amesema lengo kuu ni kurahisisha na kuelekeza jitihada za kukabiliana na athari za majanga na kuongeza ustahimilivu wa jamii, huku akiwataka vijana kushiriki kikamilifu katika kuenzi misingi ya wahasisi wa taifa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

Aidha, amesema Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na athari za majanga kabla hayajatokea kwa kuongeza uwekezaji wa rasilimali, ikiwamo ushirikiano na washirika wa maendeleo.
Ameongeza kuwa mikakati hiyo itafanyiwa tathmini kuhakikisha mipango ya maendeleo endelevu inazingatia mchango wa sekta binafsi, sambamba na kuweka mwongozo wa kisera unaoelekeza namna bora ya utekelezaji wake.
“Kwa mfano, Jiji la Mbeya linapaswa kufahamu maeneo ya makazi na majengo marefu ili kujiandaa ipasavyo kukabiliana na majanga,” amesema waziri mkuu huyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka mamlaka husika kuimarisha mifumo ya tahadhari kwa kutumia teknolojia za kisasa za ufuatiliaji na utoaji taarifa mapema, ili kusaidia wananchi kuchukua tahadhari stahiki.
Amesema pia Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ili kusaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika kuboresha sekta ya afya.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhakikisha taifa linakuwa tayari kukabiliana na maafa wakati wowote.
Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya marejeo ya Sera ya Taifa toleo la 2025, kwa kuzingatia tathmini ya utekelezaji ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Lukuvi amesema mwongozo huo utaongeza ushiriki wa wadau na uwekezaji katika shughuli za kudhibiti maafa, huku Ofisi ya Waziri Mkuu ikiendelea kuratibu utoaji wa mafunzo katika mikoa mbalimbali kuhusu namna ya kukabiliana na maafa.
Joshua Aloyce akizungumza kwa niaba ya vijana, amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu inayowaandaa kubaini changamoto za kiuchumi zinazoathiriwa na majanga katika jamii na kuhamasisha hatua za pamoja za kuyakabili.