Geita/Dar. Wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje, akijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa Chadema wamegoma kuzungumzia suala hilo huku wakieleza kwamba si kipaumbele chao kwa sasa.
Leo, Oktoba 13, 2025, Wenje ametangaza kujiunga na CCM kwenye mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Chato mkoani Geita, akipokelewa na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ndiye mgombea urais wa chama hicho.
Kutimka kwa Wenje ni pigo jingine kwa Chadema ikiwa imepita miezi michache baada ya chama hicho cha upinzani kupoteza mamia ya wanachama wake waliohamia vyama mbalimbali ikiwemo Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na kwingineko.
Vuguvugu la mtikisiko wa chama hicho lilianza wakati wa uchaguzi wake wa ndani Januari mwaka huu, uliompa ushindi Tundu Lissu kuwa mwenyekiti mpya, dhidi ya Freeman Mbowe, aliyekiongoza chama hicho kwa zaidi ya miaka 20, jambo lililosababisha mgawanyiko wa viongozi na wanachama.
Uongozi wa Lissu uliweka msisitizo wa kutoshiriki uchaguzi chini ya ajenda yake ya ‘No Reforms, No Election’, hatua iliyowakimbiza wanachama wengine ndani ya chama hicho, kwa kile alichodai kutoshiriki uchaguzi kunavunja malengo yao ya kisiasa.
Dalili za Wenje kutimka Chadema zilianza kuonekana baada ya uchaguzi huo wa Januari, kwani hakushiriki kwenye vikao vya awali vya Kamati Kuu ya chama hicho, jambo lililoibua minong’ono huku ikidhaniwa angejiunga na Chaumma kama wengine walivyofanya.
Katika maelezo yake kuhusu uamuzi wa kuhamia CCM, Wenje amesema ameona ajiunge na jukwaa hilo kwa kuwa ni sahihi kutumia maarifa yake kushauri na kuchangia maendeleo ya nchi, baada ya kudumu kwa miaka 15 ndani ya upinzani.

Amesema asingependa kubaki bila tija na maarifa aliyonayo, hivyo aliamua kujiunga na jukwaa la kisiasa linalofaa kutoa ushauri kwa ajili ya kujenga nchi.
“Mimi nikisema kabla sijafa, sitaki nife na potential nilizonazo, nije kwenye ligi kuu pahali ambapo ninaweza kutoa ushauri na pia kujenga nchi yetu. Kwa miaka 15 nimekuwa kwenye siasa, nilikuwa nacheza hizi ligi za Daraja la Kwanza, leo nimekuja kwenye ligi kuu rasmi,” amesema Wenje.
Katika hotuba yake mbele ya Samia, Wenje amesema miongoni mwa kazi muhimu zilizofanywa na CCM tangu uhuru wa nchi ni kudumisha amani na utulivu, mambo yanayoshabihiana na maendeleo.

“Kama kuna mtu anabisha aende Sudan, ajaribu Somalia, kama kuna mtu anabisha. Mheshimiwa Rais, wakati umefika, nchi imekuwa kubwa kuliko mtu,” amesema.
Wenje ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amesema ni uzushi kwa chama hicho cha upinzani kudai kimezuiwa na Serikali kushiriki uchaguzi, kwani chenyewe kupitia vikao vyake, kilikaa na kuamua kutoshiriki.
“Januari 20 mwaka huu, tulikuwa Dar es Salaam tukafanya kitu kinachoitwa Baraza Kuu la chama, likatoa mapendekezo, tukapeleka kwenye mkutano mkuu wa chama, sote tukakubaliana kwamba Chadema hatushiriki uchaguzi. Sasa nani amekukatalia kushiriki uchaguzi? Sisi tuliamua kuweka mpira kwapani, tukaogopa tukaenda,” amesema.
Baada ya uamuzi huo, amesema chama hicho kilishauriwa na wazee muhimu, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, aliyewataka wampe historia ya chama kilichowahi kufanikiwa kwa kususia uchaguzi, lakini hawakukubali.
“Chama hiki kilishauriwa na wazee mbalimbali, akiwemo Raila Odinga wa Kenya, na aliwataka wampe rejea ya chama chochote Afrika kilichowahi kuendelea kwa kususia uchaguzi,” amesema Wenje.
Amesema Taifa kama Marekani, pamoja na kuaminika kuwa ina demokrasia iliyoimarika, bado wapo wanaolalamika kuwa wanaminywa, hivyo maendeleo na demokrasia hayana ukomo.

“Duniani kote hakuna nchi ambayo imepata ukomo wa maendeleo. Leo nimekuja hapa kutoka Mwanza, mimi nimesoma Geita, tulikuwa tunatumia saa 10 kutoka Mwanza hadi Geita, leo nimetumia saa mbili,” amesema Wenje.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, amejibu kwa ufupi, akisema kipaumbele chao ni masuala yanayoendelea nchini hasa kupotea kwa watu na sio kumzungumzia mtu.
“Acheni hizo mambo, watu wanapotea halafu unataka nieleze hatua ya Wenje kuhama chama, serious…?” amehoji Heche.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Samia amesema: “Nimefurahi nimefika kituo hiki na nimepata zawadi kwa mdogo wangu Wenje ambaye tumempokea hapa. Leo nimefurahi sana, nimwambie karibu nyumbani, kwa hiyo tumempokea,” amesema Samia
Amesema mtangulizi wake, hayati John Magufuli, alikuwa kiongozi shupavu, mzalendo mwenye maono ya kimkakati, kimapinduzi huku akiwa mwalimu mzuri na mlezi mahiri kwake, ndiyo maana ameweza kukamilisha miradi aliyoacha ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, aliloliacha ujenzi wake ukiwa asilimia 37.
Samia ametaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ambapo Magufuli alifariki na kuacha ujenzi wake ukiwa zaidi ya asilimia 30, lakini sasa watu wanasafiri na vipande kadhaa vinaendelea kujengwa hadi Kigoma.