Matumizi ya simu, tablet na karatasi nyeupe yanavyoathiri macho kwa watoto

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya karatasi nyeupe, tablet na simu za mkononi yakitajwa kuwa hatari kwa afya ya macho ya watoto chini ya umri wa miaka mitatu, wataalamu wa afya wamesema usalama wa macho utategemea na muda wa matumizi.

Hivyo ikiwa atatumia muda mwingi kuiangalia karatasi kwa karibu, kadri muda unavyosonga, jicho hubadilika kimaumbile na kuanza kushindwa kuona vilivyo mbali hali inayojulikana kama ‘myopia’ au ‘short-sightedness.’

Pia, wametaja hatua za ukuaji wake, macho ya mtoto huanza kuona anapotimiza wiki tatu na huanza ukuaji wake wa kasi ikijumuisha kujiunda, kukua kuona kwa mapana mpaka miaka mitatu na huendelea hadi mitano. Baadaye hukua kwa kasi ndogo mpaka kukamilika akiwa na umri wa miaka 13.

“Macho ya mtoto mdogo bado hayajakua kikamilifu. Kuwa na muda mwingi wa kusoma au kuandika kabla ya macho kukomaa huongeza hatari ya myopia na hata uchovu wa macho. Pia ikiwa watoto wadogo watatumia karatasi nyeupe kwa karibu kwa muda mrefu zina athari kwao na ndivyo hivyo pia kwa tablet, televisheni na simu,” ameanza kwa kuelezea Rais wa Chama cha Madaktari wa Macho Tanzania, Dk Asha Mweke akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Oktoba 13, 2025.

Dk Mweke amesema mtoto anapowekwa kwenye karatasi kwa muda mrefu anazoea kuona karibu, “unazuia ukuaji wa macho kuona kwa mapana, matokeo yake akitumia sana kadri anavyokuwa anapunguza kuona kwa mbali na anabaki na uwezo wa kuona kwa karibu.”

Mkazi wa Dodoma, Rosina Albert ni miongoni mwa wazazi ambao watoto wao wanatumia miwani tiba, akisema mtoto wake alianza kusogelea televisheni kabla ya kulalamika haoni darasani.

“Alikuwa akiandika anakosea sasa kwa kuwa niko karibu na Mwalimu, nilifanya mawasiliano na tukashauriwa wazazi tumpeleke mtoto kwa daktari wa macho, akapimwa na tukashauriwa apate miwani tiba baada ya kumbaini na tatizo la kutoona mbali,” amesema.

Akisimulia makuzi ya mwanaye huyo wa kwanza (7), amesema alianza shule akiwa na miaka miwili: “Tulimwanzisha shule mapema sababu ya majukumu ya kikazi. Muda mwili alikuwa shuleni na akirudi basi nyumbani.”

Mzazi mwingine alikiri kuwa mtoto wake hutumia muda mwingi akiangalia makaratasi.

“Anachukuliwa saa 12 asubuhi akiwa shule anakuwa na madaftari na akirudi katuni na nikishafika mimi tunaanza kufanya homework akimaliza ni saa mbili usiku,” amesema mzazi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Baadhi ya walimu waliozungumza na Mwananchi wamesema watoto muda mwingi wanapokuwa shuleni, hujifunza kuchora na kupaka rangi picha na namba pamoja na kwamba, mafunzo hayo yote hutumia daftari, karatasi na penseli na rangi.

“Ubaoni huanza kujifunza wakiingia awali, mwanzo huanza kwa kuchora na wengine wanatumia tablet ambazo huwafunza kuhesabu na kuonesha maumbo ya vitu,” amesema mmoja wa walimu hao ambao hawakutaka kutaja majina.

Alipotafutwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Suleiman Ikomba amesema ingawaje wao husimamia zaidi walimu wa umma, mafunzo ya njia za kielektroniki yana miongozo yake.

“Watoto wana muda maalumu wa kukaa darasani na kufundisha kwa njia ya skrini ni kukaa umbali mrefu anayeelekeza ni mwalimu, wanamwangalia wakiwa kwa umbali ule unaotakiwa,” amesema Ikomba.

Makamu Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi (Tamongosco) Taifa, Mathew Alex amesema wamekuwa wakiwahimiza wanachama wao kufuata miongozo iliyowekwa kwenye kudahili muda sahihi wa kuanza darasa la awali na chekechea.

Amesema elimu itolewe kwa wazazi wajue makuzi ya watoto na masharti ya usajili yakazwe zaidi shule ziwe na miundombinu, watoto wacheze zaidi.

“Nakubaliana nao madaktari kwa asilimia 100 kinachochangia watoto hawa kukaa muda mrefu darasani na kushindwa kuyapa macho yake mazoezi ni mengi yanachangiwa na wazazi pia na mtindo wa maisha,” amesema Alex.

Daktari wa macho, Mweke amesema karatasi nyeupe haina tabu sana lakini ule mwanga unaingia sana jichoni, na mtoto anatumia umbali mfupi kuangalia kitu kwa muda mrefu hivyo huchangia pia kuathiri macula.

Amesema mzazi atamtambua mtoto ambaye anafinya sana macho au anasogea karibu na TV ni kiashiria uwezo wake wa kuona mbali umepungua.

Mweke amesema ni muhimu mtoto kukutana na mwanga na eneo lenye urefu unaofaa ili kuanza kuyashughulisha macho yake na kwamba haishauriwi watoto kutumia vifaa vya kielektroniki.

Dk Mweke ameshauri mtoto aangalie TV ndani, “masaa mawili aachwe acheze nje kusaidia ‘mapana’ yake (uwezo wa macho yake kukua kuona mbali).

“Karne ya Uviko-19 ilitulazimu watoto kutumia tablet lakini ile ndiyo mbaya zaidi na inaleta athari zaidi ya mionzi,” amesema.

Mtaalamu wa macho Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songwe, Dk Otilia Ngui amesema mtoto anapoachwa kwa muda mrefu ndani achezee au akae na vitu vya kuangalia karibu anaweza kupata changamoto kwa kuwa, anakuwa ameshika umbali mfupi sana.

Na ikiwa muda mwingi atakuwa kwenye TV, basi macho yake yatapata changamoto mapema na ikiwa ni simu ni hatari zaidi kwani mikono yake ni mifupi hivyo simu itakua karibu zaidi na macho.

“Simu inasababisha kutoona vitu vya mbali vizuri, watoto wawekwe nje ya uwanja wanacheza anayekaa ndani mara nyingi anakuwa na matumizi ya simu sana, anakuwa amejikita pale changamoto inayowafanya wasione vizuri mwanzoni au baadaye atakapokuwa amekua,” amesema Dk Ngui.

Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio amesema watoto chini ya mwaka mmoja haitakiwi kutumia kabisa simu, huku akisema wazazi ndiyo kipindi hukazana kuwatafutia tablet.

Amesema hiyo imesababisha ongezeko la watu wenye uhitaji kutumia miwani tiba.

 “Muda wote mtoto kuwekwa ndani kunasababisha waweze kuona karibu tu uwezo wa kuona mbali unashindwa kujengeka, mazoezi ya kuona mbali yanamfanya aone mbali zaidi anapoendelea kukua matokeo yake watahitaji miwani tiba,” amesema.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema takwimu za mwaka 2024, jumla ya watu milioni 1.5 walihudumiwa kwenye kliniki za macho nchini, ambapo asilimia 42 walikuwa watoto chini ya miaka 15.

Kati ya watoto hao, asilimia 6.3 walifika wakiwa tayari na ulemavu wa kutokuona.

Amesema kwa mwaka 2025 jumla ya huduma mkoba 59 zimefanyika katika maeneo mbali mbali nchini na jumla ya wananchi 132,107 wamefikiwa na kupatiwa huduma katika maeneo yao wanayoishi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeimarisha huduma za macho katika hospitali za kanda na Taifa, mwaka 2024 pekee zaidi ya watoto 1,000 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na kupatiwa miwani, sawa na asilimia 55.6 ya wahitaji waliolengwa.

Dk Magembe amesema tafiti zinaonesha kuwa, mtoto mmoja kati ya watoto 1,000 ana ulemavu wa kutokuona na watoto katika nchi zenye uchumi wa chini na wa kati wako katika hatari mara mbili hadi tano zaidi ya kushindwa kuhudhuria shule kutokana na matatizo ya macho.

Amesema hali hiyo inasababisha changamoto kubwa katika elimu, ajira, na ushiriki wa kijamii kwa watoto na vijana wengi ulimwenguni.

“Hapa nchini, inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 12 wanahitaji huduma za afya ya macho. Magonjwa yanayoongoza ni pamoja na mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho kuona mbali au karibu unaorekebishika kwa miwani, shinikizo la macho, madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye pazia la jicho pamoja na mzio na maambukizi ya macho,” amesema Dk Magembe.

Amesema magonjwa hayo yanarudisha nyuma maendeleo ya familia, jamii na Taifa kwa jumla.