Hatutumiwi na Serikali, Tunahubiri Uzalendo na Amani – Video – Global Publishers


Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, amesema Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) litaendelea kusimamia maslahi mapana ya taifa, huku akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwa wazalendo na kulinda amani iliyopo nchini.

Akizungumza Oktoba 12, 2025 mkoani Njombe wakati wa ziara yake ya kikazi, Mufti Zubeir alisema jukumu kubwa la BAKWATA ni kuhimiza amani, umoja na uzalendo miongoni mwa wananchi, si kama baadhi ya watu wanavyodhani kwamba baraza hilo linatumiwa na serikali.

“Tunahubiri sana kuhusu amani na uzalendo kwa sababu tunaijua nchi ilivyo sasa. Wapo wanaofikiri sisi ni vibaraka, kwamba serikali inatutumia kusema jambo fulani. Hapana, hatutumiwi na serikali. Tunajua umuhimu wa kutengeneza jamii inayojua thamani ya kuwa mzalendo katika nchi yake,” alisema Sheikh Mkuu.

Amesema BAKWATA imekuwa ikishirikiana na serikali na taasisi mbalimbali katika kulinda amani na kukuza maadili mema ya kijamii, jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote bila kujali itikadi zao.

Mufti pia alisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, hivyo kila raia ana wajibu wa kuhakikisha inalindwa kwa vitendo na si maneno pekee.

“Kama taifa halina amani, hakuna ibada, hakuna elimu, hakuna maendeleo. Ndiyo maana sisi kama viongozi wa dini tunalizungumzia hili mara kwa mara, kwa sababu tunatambua uzito wake,” aliongeza.

Ziara ya Mufti Zubeir mkoani Njombe inalenga kukutana na viongozi wa dini, serikali, na jamii kwa ujumla, kwa madhumuni ya kuimarisha umoja na mshikamano wa kidini na kitaifa.