Dar es Salaam. Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliamini kwa dhati kwamba elimu ni nyenzo kuu ya ukombozi wa binadamu.
Kwa Nyerere, elimu haikuwa tu njia ya kupata ajira, bali ilikuwa chombo cha kumkomboa mtu kutoka kwenye ujinga, umaskini na utegemezi.
Alisisitiza kuwa elimu inapaswa kumwezesha mtu kufikiri, kuwa huru katika uamuzi, na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii yake.
Katika maandiko na hotuba zake nyingi, Nyerere alieleza wazi kuwa elimu inapaswa kujikita katika mazingira ya Mtanzania na iwe na lengo la kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla, si mtu binafsi pekee. Alikosoa mifumo ya elimu ya kikoloni kwa kusema kuwa ililenga kuwatayarisha watu wachache kwa ajili ya kazi za ofisini badala ya kuwatayarisha kuwa raia waliokomaa, wenye maarifa ya kuchangia maendeleo ya taifa lao.
Aliwahi kusema: “Elimu yoyote inayojenga kuta kati ya wahitimu wake na jamii wanamoishi si elimu ya kweli.” Hii ni nukuu inayoakisi mtazamo wake kwamba elimu ya kweli ni ile inayomfanya mtu aende kwao vijijini na kutumia alichojifunza kuboresha maisha ya jamii yake.
Nyerere alipendekeza mfumo wa elimu unaojulikana kama “Elimu ya Kujitegemea”, ambao ulilenga kujenga taifa linalojitegemea kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Katika waraka wake maarufu wa mwaka 1967 uitwao “Education for Self-Reliance”, alieleza kuwa elimu inapaswa kumsaidia mwanafunzi kuelewa dunia inayomzunguka, kuweza kutumia maarifa yake kutatua matatizo halisi, na kujifunza kuwa sehemu ya jamii anayohudumia.
Katika waraka huo aliandika: “Elimu yetu haipaswi kutufanya tuwe watawala wa watu wetu, bali watumishi wao.”
Kauli hii inaonyesha wazi kuwa Nyerere alitaka elimu ijengwe juu ya misingi ya usawa, utu, na mshikamano wa kijamii.
Kwa Nyerere, elimu ilikuwa pia njia ya kuimarisha maadili. Aliamini kuwa raia mwenye elimu anapaswa kuwa mkweli, mwadilifu, na mwenye moyo wa kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya wengine.
Aliogopa elimu inayomfanya mtu kujiona bora kuliko wengine au kutaka kujinufaisha binafsi kwa gharama ya wengine. Hivyo basi, aliendelea kusisitiza kuwa mfumo wa elimu lazima ujengwe kwa namna, ambayo unawafanya wahitimu wawe na moyo wa kizalendo, si wa kimaslahi binafsi.
Aidha, Nyerere hakuona elimu kama jambo la kifahari au kwa wachache, bali haki ya kila Mtanzania. Alisema; “Si haki kwamba baadhi ya watoto wapate elimu bora kwa sababu tu wamezaliwa mjini au kwa wazazi wenye uwezo.”
Hili lilisababisha serikali yake kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuzi wa elimu ya msingi na kupambana na ujinga, hasa vijijini. Aliamini kuwa hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana bila kuwaelimisha watu wengi zaidi.
Kwa ujumla, falsafa ya Nyerere kuhusu elimu ilikuwa ya kipekee na ya mbele zaidi kwa wakati wake. Aliiona elimu kama mchakato wa kuunda jamii huru, yenye uwezo wa kufikiri na kuchukua hatua kwa faida ya pamoja. Mtazamo huu unaendelea kuwa msingi muhimu wa mijadala ya elimu nchini Tanzania hadi leo.