Arusha. Naona ni jambo jema nikukaribishe msomaji tujiulize pamoja swali hili: Je, nina elimu kiasi gani? Nina maarifa kiasi gani?
Ni kama vile mtu anajiuliza: nina hela kiasi gani mfukoni kwangu? Au nina fedha kiasi gani katika akaunti yangu huko benki au katika simu yangu?
Hivyo ni jambo jema, tena la busara, kutafakari juu ya kina na mapana ya elimu na maarifa tuliyonayo.
Kuna methali hizi mbili za Kiswahili: Elimu ni bahari haishi kwa kuchotwa. Na hii ya pili: Elimu haina mwisho.
Pamoja na uwepo wa methali hizi, na mifano mingine katika maisha inayotuonyesha kwamba hatujui kila kitu, bado mara nyingi tunatamba kwamba tuna elimu na maarifa kushinda watu wengine. Yaani tuna ile tabia ya kujisikia kuwa wajuaji. Tunajisikia kuwa wataalamu na wabobezi.
Mawazo haya na tabia hii yaweza kumfanya mtu akadhani kwamba ana maarifa mengi sana na anajua mengi sana.
Pia tuna tabia ya kudhani kwamba mtu fulani anajua mambo mengi sana, hasa kama amepitia shuleni kwa muda mrefu.
Na kama huyo mtu ana shahada ya uzamili basi anaweza kujisikia kwamba anajua mengi sana, hasa pale wanaomzunguka wanaamini kwamba huyu ndugu yao ni msomi anayejua mengi sana.
Tutafakari
Hebu tutafakari jinsi tunavyowaona wale walio na shahada ya uzamivu, shahada ya Udaktari au Ph D. kwa Kiingereza.
Utasikia mtu anasema: mimi nimefikia shahada ya udaktari, ni msomi sana. Na walio wengi mno kati yetu tunaamini kwamba hawa ni wasomi, wabobezi, wataalamu.
Katika hili la “elimu ni babari” huwa mara nyingi napenda kutafakari juu ya safari yangu binafsi katika kusaka elimu na maarifa.
Nikiwa sasa katika kile unachoweza kukiita umri mkubwa, natafakari kuhusu maarifa na elimu niliyonayo kama profesa wa falsafa.
Ninayoyaona yananishangaza. Nimejikuta nafikiria hivi: kama mtu una swali la kuniuliza, ungepaswa kuniuliza swali hilo zamani nilipokuwa mwalimu wa sekondari, na hasa baada ya kupata shahada za uzamili katika theolojia na elimu na falsafa.
Wakati huo “nilifahamu kila kitu.Nilijibu kila swali la kila mwanafunzi bila tafakari kidogo tu kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba sikuwa na majibu sahihi.
Hilo halikuingia kichwani kwangu. Ati kwamba mtu niliyesoma hadi kupata shahada Marekani sikuwa na jibu kwa swali fulani? Hiyo haikuwepo.
Mbona nilijua kila kitu? Wakati huo nilidhani kwamba mtu kusema sijui au sina uhakika na ninachokijua kuhusu jambo fulani, ni kuonyesha ujinga. Ni kuonyesha kwamba sina maarifa ya kutosha.
Ndiyo maana nasema kama una swali lolote kwangu, niulize wakati nilipokuwa kijana zaidi, kwenye miaka ya 1970 hadi karibu na miaka ya 2000.
Hapo nilijua kila kitu. Nilikuwa “msomi”, mjuaji, mtaalamu! Ukiwa na swali, niulize kipindi hicho.
Mawazo hayo potofu yalianza kuyeyuka kiasi fulani wakati wa kusoma shahada ya uzamivu na hasa katika kufanya utatifi unaotakiwa katika masomo ya shahada hiyo.
Ndipo nilipoanza kuona kwamba kweli elimu ya falsafa ni bahari ambayo haiishi kwa kuchotwa. Hapa sizungumzii elimu za aina nyingine: nazungumzia tu: elimu na maarifa katika falsafa. Lo, ajabu ya Musa!
Kila nilipofanya utafiti zaidi, ni kiasi hicho nilitambua kwamba nilichojua katika falsafa kilikuwa sehemu ndogo sana katika maarifa ya somo la falsafa.
Yaani nasema hivi: nilianza kutambua kwamba kile nilichojua katika falsafa kilikuwa kama tone katika bahari ya somo pana la falsafa.
Ni wakati huo nilianza kutambua kwamba elimu niliyokuwa nayo ilikuwa sehemu ndogo sana ya maarifa yaliyo duniani.
Ni wakati huo, na pia ni wakati huu wa sasa, nimeanza kujua ukweli wa methali hii: Elimu ni bahari, haishi kwa kuchotwa.
Na ndiyo maana nasema: ukiwa na swali la kuniuliza, niulize nilipokuwa na umri kati ya 20 na 70 kwa sababu wakati huo nilijua kila kitu. Kwa sasa najiona kwamba kile ninachojua katika falsafa ni kidogo sana kulingana na falsafa kwa ujumla. Na hapa nazungumzia falsafa tu, sizungumzii masomo na fani nyingine.
Wengine wajiulize
Kama ni hivyo ilivyo kwangu ninayeendelea kila siku kujifunza, kutafiti, kutafakari, kuandika, na kufundisha somo hili, na kujikuta najua kidogo sana katika falsafa, itakuwaje katika fani nyingine?
Mbona huko mimi si mtaalamu hata kidogo? Mimi sina utaalamu katika fani nyingine nyingi mno. Nina utaalamu kidogo sana katika falsafa.
Mara nyingi rafiki zangu na wanafunzi huniambia: wewe ni profesa, hebu nijibu swali hili: kisha ananipa swali linalohusu uchumi au ufugaji.
Ni kama kusema profesa anajua kila kitu. Si kweli. Huenda akajua mengi katika fani yake, na huenda anajua machache katika fani nyingine, lakini hajui kila kitu.
Ukweli ninaotambua sasa ni huu: kile ninachojua ni kama nukta katika elimu iliyo duniani. Soma vizuri. Nimesema: NUKTA. Yaani hii alama ya . (nukta) inaonyesha jinsi elimu tuliyo nayo ilivyo ndogo katika picha ya elimu na maarifa yaliyo duniani.
Hivyo basi, wale tunaodhani tunajua sana, au tumesoma sana, au tumekuwa viongozi kwa muda mrefu, tutambue bila shaka kwamba tunachokijua ni tone katika bahari ya maarifa na elimu.
Tutambue kwamba ni busara kuu kutambua kwamba wapo wengine walio wataalamu zaidi katika fani fulani.
Kama mtu umepata elimu ya chuo kikuu na kupata shahada kubwa, ni busara kutambua kwamba hujui kila kitu.
Ukiwa kiongozi uwe mnyenyekevu na uwe tayari kumsikiliza kila mtu. Analo la kukufundishe wewe unayetamba kwamba una shahada ya uzamili au uzamivu.
Nakumbuka busara aliyonifundisha mama mzaa baba yangu: una masikio mawili na mdomo mmoja, hivyo sikiliza sana na ongea kidogo. Huu upeo wa uelewa wa bibi yangu unanishangaza kila siku mimi ninayejiona kwamba nimesoma sana: ati nina shahada ya udaktari.
Kwa hili, na mengine mengi ya busara katika maisha, bibi amenipita sana. Anastahili kuwa na shahada nilizo nazo.
Nimetambua bila shaka yoyote, kwamba ninachokijua sasa ni nukta tu katika maarifa yaliyo duniani.
Kama una swali kwangu, uniulize wakati nilipojua kila kitu. Sasa najua kidogo sana. Swali lako mpe mtu mwingine.
Prof. Raymond S. Mosha
(255) 769 417 886; [email protected]