Idara ya Uhamiaji nchini imewaondosha raia wawili wa kigeni waliobainika kukiuka masharti ya viza zao za matembezi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 14, 2025 na Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, wageni hao walioondolewa jana, Oktoba 13, 2025, ni Dk Brinkel Stefanie, raia wa Ujerumani mwenye hati ya kusafiria namba C475MMNGL na Catherine Janel Almquist Kinokfu, raia wa Marekani mwenye hati ya kusafiria namba A80321764.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa hatua ya kuwaondosha nchini imechukuliwa baada ya kubainika kuwa walikiuka masharti ya viza zao za matembezi, jambo lililo kinyume na taratibu zilizowekwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 pamoja na kanuni zake.
Idara ya Uhamiaji imewataka raia wa kigeni wanaoingia na kuishi nchini kuhakikisha wanazingatia masharti yaliyoainishwa katika viza au vibali vyao vya ukaazi, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza pindi wanapokiuka sheria.
“Tunatoa wito kwa raia wa kigeni kuzingatia matakwa ya viza zao kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wowote,” amesema Mselle katika taarifa hiyo.
Idara ya Uhamiaji imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya wageni nchini na kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka sheria za uhamiaji.