Mabeki Simba kikaangoni, Pantev akipewa dawa

MECHI mbili za kirafiki ilizocheza Simba dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikianza na ushindi wa mabao 2-1 kisha ikachapwa 4-1 zimewaibua mastaa waliowahi kukipiga katika kikosi hicho ambao wamewaonya wenzao wakati huu wanapojiandaa kukipiga dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba inaifuata Nsingizini nchini humo keshokutwa kwa ajili ya mechi ya awali ya mzunguko wa pili wa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam ambapo Simba iliifunga Al Hilal mabao  2-1 wafungaji wakiwa ni Jonathan Sowah na Jean Charles Ahoua na ile ya pili ilifungwa  4-1 kwenye Uwanja wa Gymkhana mfungaji pekee wa Wekundu akiwa ni Elie Mpanzu.

Kutokana na matokeo hayo, beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah amesema benchi la ufundi la timu hiyo limepata kipimo kizuri kabla ya kucheza na Nsingizini Hotspurs, lakini linachopaswa kufanya ni kuhakikisha kwamba makosa yanafanyiwa kazi haraka na kwa ufasaha.

MABE 01

“Al Hilal pia inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika imeisaidia Simba kusahihisha makosa kabla ya mechi yao ya Jumapili itakayopigwa ugenini dhidi ya Nsingizini. Eneo la kwanza ninaloliona linatakiwa kufanyiwa marekebisho ni mabeki maana mechi mbili wameruhusu mabao matano,” amesema Maftah na kuongeza:

“Natambua kuna wachezaji wapo katika timu zao za taifa, lakini haijalishi wanatakiwa wachezaji wote wawe na uwiano wa kiwango (bora)… kupitia mechi hizo makocha wamejua kipi wakifanye.”

Beki wa zamani wa Yanga na Stars, Oscar Joshua amesema: “Mechi za kirafiki zinawasaidia makocha na wachezaji kujua kikosi kina ubora na upungufu gani, hivyo Simba itakuwa na wakati mzuri wa kujipanga zaidi kabla ya mechi yake ya CAF.”

Hata hivyo, kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni amesema pamoja na maboresho, lakini mkocha na wachezaji wanapaswa kujiangalia katika eneo la kujilinda ili kutoruhusu mabao kizembe.

MABE 02

“Mechi za kirafiki zinawasaidia makocha kutambua kikosi chake ni cha aina gani pia kwa Pantev (Dimit ambaye ni meneja) atapata wakati mzuri wa kumfahamu kila mchezaji ana uwezo gani,” amesema na kuongeza:

“Safu ya mbele inafunga ndiyo maana Sowah, Mpanzu na Ahoua (Jean) wote wamemuonyesha kocha wana uwezo wa kutumia nafasi, kikubwa waangalie namna ya timu kuwa imara katika kujilinda.”

Msimu uliopita Sowah akiwa Singida Black Stars alikosajiliwa dirisha dogo alifunga mabao 13 huku Ahoua alikuwa kinara wa mabao 16 asisti tisa katika Ligi Kuu Bara ilhali Mpanzu alifunga mabao manne na asisti sita.