Hersi: Umri ulisababisha nisiaminike Yanga

RAIS wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema wakati anaanza kuiongoza klabu hiyo, wengi hawakumuamini kutokana na umri wake mdogo.

Hersi amesema wakati anaanza kuongoza Yanga watu wengi walipata mashaka kutokana na kwamba alikuwa ndiye kiongozi pekee mwenye umri mdogo huku mwenyewe akikubali wasiwasi wao.

“Niliwaelewa wale ambao walikuwa na wasiwasi na umri wangu, nilikuwa kiongozi mwenye miaka thelathini flani hivi, lakini kwangu haikuwa shida, nilijipanga kuitendea haki nafasi hii,” amesema Hersi.

“Niliaminiwa na watu wakubwa ambao walikuwa kwenye Baraza la Wadhamini wakiwemo mzee wangu Mkuchika (George) nikajipanga na Kamati ya Utendaji yangu kwamba tuna kazi ya kufanya kuwathibitishia watu kwamba inawezekana.”

Aidha Hersi ametoa wito kwa vijana kuhakikisha wanapoaminiwa wanatakiwa kufanya kweli kwa kutengeneza historia bora kama ambavyo amefanya.

“Vijana wengi wamekuwa hawazitendei haki nafasi ambazo wamekuwa wakizipata, wapo vijana wengi wanaweza kufanya makubwa lakini wanahitaji kutanguliza weledi,” amesema Hersi.

Hersi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 14, 2025 katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar, ikiwa ni siku chache baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Klabu FIFA. Pia Hersi ni Mwenyekiti wa Klabu barani Afrika.

Ikumbukwe kuwa, Julai 9, 2022, ilikuwa siku ya kihistoria kwa mashabiki na wanachama wa Yanga baada ya kumchagua Hersi kuwa rais wa klabu hiyo, huku akiwa ni mgombea pekee katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Hersi alichaguliwa kuwa kiongozi wa juu wa Yanga baada ya Mshindo Msolla kumaliza muda wake wa uongozi aliodumu kuanzia 2019 hadi 2022.