Ruhangwa. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi na Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi akipewa ridhaa na wananchi kuongoza nchi, atamtumia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kuendesha nchi.
Mwalimu ametoa ahadi hiyo katika Kijiji cha Mikenyela Jimbo la Ruangwa, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake katika mikoa ya Kusini zilizoingia siku ya pili, akitafuta kura za wananchi katika ukanda huo.
Katika hotuba yake kwa wananchi hao, pamoja na mambo mengine, amemtja waziri mkuu ambaye amekuwa madarakani kwa miaka kumi na kuwa kwa uzoefu wake, akishika dola, hataacha kumtumia.

“Nampongeza sana Waziri Mkuu Majaliwa na niahidi, hata nikishinda, siwezi kumuacha pembeni kwani inasikitisha pamoja na kuwa Waziri Mkuu miaka 10 na kazi kubwa alizozifanya, kuna wachache leo wanambeza.
“Nimhakikishie, nikiwa Rais nipo tayari kufanya naye kazi na nitalinda masilahi yake, siendi kufukua makaburi Ikulu kwani hakuna mkamilifu, ni binadamu, alikosea kama binadamu mwingine,” ameeleza Mwalimu.
Mwalimu ameongeza kuwa huenda kwenye kipindi chake kama Waziri Mkuu ndio atakwenda kula bata zaidi kwa kuwa hata katika nchi mbalimbali atakazokuwa anazunguka, atakwenda naye.
Pia, katika masilahi yake ya kuitumikia nchi, amesema atahakikisha anayasimamia na kuishi vizuri katika kipindi chote atakachokuwepo hapa duniani.
Mbali na kumzungumzia Majaliwa, pia Mwalimu amesema katika Jeshi la Polisi, atakwenda na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura na kufanya naye kazi hadi pale atakapostaafu.
“Nikiapishwa, Wambura ataendelea na nafasi yake ya IGP mpaka atakapostaafu na hii siyo kwake tu, bali hata kwa makamanda wengine, kwani kikubwa ninachotaka kukifanya ndani ya jeshi hilo ni kuliboresha kidogo.
“Kwenye uongozi wangu, si Majaliwa tu na wengine wote walio serikalini, sina mpango wa kufukua makaburi, tutatengeneza maridhiano ili twende mbele kama Taifa.
“Dhamira yangu kwa JeshI la Polisi ni kwenda kuliboresha na kwa wale wachache wanaolichafua basi wachukuliwe hatua, ili tuwe na jeshi madhubuti kwa ajili ya kulinda raia na mali zao na siyo liwe paka na chui na wananchi,” amesema.
Mwalimu ameongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likifanya kazi nzuri na linapaswa kupongezwa.
“Nakwenda kujenga nchi yenye mshikamano wa dhati, siendi kunyonga mtu kwa kumwambia kuwa wewe ulionea watu. Sina mpango wowote wa kwenda kulipa kisasi Ikulu,” amebainisha mgombea huyo.
Akiwa Wilaya ya Nachingwea, Mwalimu amesema kwa namna nchi inavyoendeshwa sasa, haoni umoja na mshikamano aliouacha Mwalimu Julius Nyerere.
Amesema kipindi cha Mwalimu Nyerere, katika kudumisha umoja na mshikamano, hakukuwa na utoaji huduma za kubagua watu, lakini leo kuna shule na hospitali binafsi huku huduma zikitofautiana kwa kiasi kikubwa.
“Enzi za Mwalimu hakukuwa na shule za binafsi wala hospitali, hali iliyofanya tusome na watoto wa mawaziri, lakini leo hii, hata mtoto wa mkuu wa wilaya au mkuu mkoa hawezi kusoma shule zetu na hivyo kuchangia utoaji elimu kuwa mbaya,” amesema Mwalimu.
“Mkitupa ridhaa ya kuongoza nchi, nakwenda kudumisha umoja na mshikamano kwa kuhakikisha huduma zote zinatolewa kwa usawa, kwani hatuwezi kumuenzi Baba wa Taifa wakati umasikini unaongezeka, huduma za kijamii zinadorora, hii sio nchi aliyotuachia,” amesema.
Pia, amesema wakati Mwalimu Nyerere anaimba wimbo wa umoja na mshikamano, alikuwa akiendeleza nchi ikiwemo uanzishwaji wa viwanda mkoani Tanga na ujenzi, lakini leo vyote hivyo vimekufa.
Vilevile, amesema Mwalimu Nyerere hakuwa anauza gesi wala kuanza kuchimba mafuta, lakini kulikuwa na ahueni ya maisha katika mikoa ya kusini ikiwemo kutegemea kilimo.
“Leo Lindi mna bahari, gesi, mafuta na korosho ambazo dunia inazichukulia kama dhahabu lakini mnatawaliwa na umasikini na kutoona maana ya kuwa na rasilimali hizo, naomba chagueni Chaumma tuwaletee mabadiliko,” amesema Mwalimu.
Katika suala la uchumi, mgombea huyo amesema kwa yeye ni muumini wa biashara huru, katika uongozi wake, hakutakuwepo na uuzaji mazao kwa njia ya stakabadhi isipokuwa kila mtu atakuwa huru kuuza kule anapona kunamfaa.
“Stakabadhi ghalani katika kuuza korosho ni uhuni, acha watu wauze korosho wanavyotaka, niwahakikishie, katika kutatua hilo kwenye uongozi wangu, kilo moja ya korosho itafika Sh10, 000 kwani ukweli ni kwamba inahitajika duniani na madalali hawawezi kutupangia bei,” amesema Mwalimu.