Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata watu 76 wanaotuhumiwa kuvamia, kuvunja maduka, nyumba, kuiba vyuma na kuviuza kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu kinyume na sheria.
Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni iliyotekelezwa kuanzia Oktoba 11 hadi 14, 2025 katika wilaya za Nyamagana na Ilemela, mkoani Mwanza, imebaini kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaotuhumiwa kununua vyuma hivyo huku wakijua vimepatikana kwa njia ya wizi.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Oktoba 14, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa
“Tumekuwa tukipata taarifa za matukio ya uhalifu kutoka kwa wananchi kuhusu uwepo wa makundi ya uhalifu yanayohusisha vijana wanaookota makopo na kutembea kwa makundi ya kuanzia watu saba hadi 15 na kwenda kwenye maduka kuvunja na kung’oa vyuma. Pia, tumekamata watu wanaopokea mali hizo,” amesema kamanda Mutafungwa.
Amesema kati ya watuhumiwa hao 76 waliokamatwa, 13 wamekutwa na mali zinazodhaniwa ni za wizi, 25 wamepatikana wakiwa na dawa za kulevya, 11 wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya ukahaba na 22 wakituhumiwa kucheza kamari.

”Katika oparesheni hii maalumu wamepatikana vijana 16 wanaofanya kazi za kuokota makopo na vyuma chakavu kisha kujihusisha na uhalifu, kukiuka masharti ya leseni za biashara, kupatikana na pombe ya moshi, kufanya fujo na kupatikana na mali ya wizi,” amedai Mutafungwa.
“Vilevile, tumekamata vielelezo mbalimbali vya kufanyia uhalifu ambavyo ni pikipiki tatu ambazo wamiliki hawana uhalali wa kuzimiliki kisheria na zinatumika katika matukio ya uhalifu, mtungi mmoja wa gesi, nondo, betri za gari, mizani miwili ya kupimia, madumu 15 ya petroli na dizeli, ufuria kubwa mbili na simu aina mbalimbali.”

Kamanda huyo amesema watuhumiwa 11 wanaojihusisha na biashara ya ukahaba, wanatuhimiwa pia kushiriki kwenye matukio mengine ya uhalifu kwa kushirikiana na wahalifu mbalimbali.
“Pia, askari wetu katika misako hii wamepita kwenye nyumba za kulala wageni kufuatilia matukio ya uhalifu, baadhi ya wafanyabiashara wamekamatwa kwa kukiuka leseni zao za biashara,” amesema Kamanda huyo
Mutafungwa amesema operesheni hizo ni endelevu huku akiwapongeza wananchi wa mkoa huo kwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.
“Wananchi waendelee kuliamini Jeshi la Polisi wajitokeze na kutoa taarifa kwa maofisa wetu kuanzia ngazi ya kata ili zifanyiwe uchunguzi na kuwakamata wahalifu wote,” amesema Mutafungwa.