Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania na bingwa wa marathoni taifa upande wa wanawake, Koplo Magdalena Shauri amerejea nchini akitokea Marekani alikokwenda kushiriki mbio za Chicago Marathon.
Mbio hizo zilifanyika Oktoba 12, mwaka huu jijini Chicago, ambapo Magdalena alimaliza wa tatu kwa muda wa 2:18:03 na kuwa Mtanzania wa kwanza kumaliza tatu bora katika mashindano hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977.
Nyota huyo ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya taifa ya muda wa saa 2:18:41 aliyoiweka 2023 kwenye Berlin Marathon, alionyesha ubora na uthabiti mkubwa kwa kuivunja, huku akiiboresha kwa sekunde 38 kutoka saa 2:8:41 hadi 2:18:03.

Akizungumza wakati wa kumpokea mwanariadha huyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya Utimamu wa Mwili na Michezo iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha, Kanali John Nyanchoa akiiwakilisha makao makuu ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amempongeza Magdalena kwa jitihada za kuitangaza nchi kimataifa kupitia michezo.
Amesema Magdalena ni mtu ambaye anajituma, mwaminifu na mwadilifu jambo ambalo limemfanya aendelee kung’ara katika mashindano mbalimbali ambayo amekuwa akishiriki.

Kanali Nyanchoa ameongeza kuwa kama jeshi na Taifa ni jambo la kufurahia kuona mwanariadha anafanya vizuri kimataifa.
“Nipende kuwapa moyo wanariadha wengine wafanye mazoezi kwa kujituma na kuwa na nidhamu katika michezo ili kuja kuliletea taifa sifa kubwa kama alivyofanya,” amesema
Ameweka wazi kuwa ushindi wa Chicago kwa Magdalena ni kwa nchi ya Tanzania na kuongeza kuwa utii wake na kukubali kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi ndio siri ya mafanikio.

“Pongezi kwa mkuu wetu wa Majeshi, Jenerali Jacob John Mkunda kwa sababu yeye ndiye anatoa nafasi kwa wanajeshi wana michezo kushiriki michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa sababu ametoa muda wa kutosha kwa vijana hawa na hawapangiwi majukumu yoyote zaidi ya kufanya mazoezi,” amesema Nyanchoa.
Meja Didas Msholwa ni kaimu kamanda wa kikosi 977 Rejimenti, kikosi ambacho anatokea Magdalena Shauri, naye amempongeza kwa juhudi zake mpaka ameweza kupata ushindi huo mkubwa ambao unaitangaza nchi.

“Kama tulivyoona siku chache zilizopita kulikuwa na ushindi wa Alphonce Simbu. Kwa hiyo hii ni chachu ambayo inasababisha na wengine kufanya vizuri,” amesema Msholwa.
Meneja wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Usu Jonas Fabian amewataka wanariadha wengine kuiga kile ambacho amekifanya Magdalena.
“Ni ushindi wa Taifa na ni ushindi wa jeshi kwa hiyo Magdalena atazidi kuleta ushindi mkubwa na nina imani siku moja ataleta medali ya dhahabu kwa nchi yetu,” amesema Fabian.
Naye kocha wa timu ya riadha ya JWTZ, Mteule Daraja la Pili Antony Mwingereza amesema siri ya Magdalena kufanya kweli Chicago ni kujituma kwa bidii kwenye mazoezi kwa kushirikiana na wenzake na pia kumtanguliza Mungu kwenye kila jambo ambalo anafanya.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Stephen Akhwari amesema rekodi mpya ya nyota huyo itakwenda kuongeza hamasa na morali kwa wanariadha wengine hasa wa kike.
Kwa upande wake Magdalena amesema kuwa mbio hazikuwa rahisi kutokana na ushindani uliokuwepo na wanariadha kutoka mataifa mengine ambao walishiriki.
Amesema kilichombeba ni mazoezi ambayo alifanya kwa muda mrefu.