Ujenzi daraja la sita kwa urefu nchini wafikia asilimia 74.3

Tanga. Ujenzi wa Daraja la Pangani mkoani Tanga lenye urefu wa mita 525 pamoja na barabara unganishi na mchepuko zenye jumla ya urefu wa kilomita 25, umefikia asilimia 74.3 hadi kufikia Septemba 30, 2025.

Kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa kuta mbili unganishi za daraja (abutments) na nguzo nane za kati (piers), huku jumla ya Sh45.6 bilioni zikiwa zimeshalipwa kwa mkandarasi.

Ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya dhamira kuu ya Serikali katika kufungua na kuunganisha Mkoa wa Tanga na ushoroba wa Ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Malindi – Mombasa – Lunga Lunga/Horohoro – Tanga – Pangani – Bagamoyo (Makurunge) wenye urefu wa kilomita 454.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 14, 2025 na Meneja wa  Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Msama, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

 Amesema kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa kupunguza muda wa usafiri, kurahisisha biashara, kuwezesha wananchi kuchangamana, kuongeza ufikikaji wa vivutio vya utalii, na kuwa kiungo kati ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa – hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu.

Mhandisi Msama ameongeza kuwa ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (kilomita 50), ambayo ni sehemu ya kwanza ya mradi huo, unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na kutekelezwa na Tanroads. Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya Chico kutoka China, na utekelezaji wake umefikia asilimia 75.

Sehemu ya pili ni ujenzi wa Daraja la Pangani na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 25.6, unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Sehemu ya tatu ni ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange yenye urefu wa kilomita 95.2, ambayo imefikia asilimia 53 ya utekelezaji na itagharimu Sh94.538 bilioni.

Aidha, amesema barabara hiyo itawawezesha wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo hususan mihogo, nazi na mwani, hivyo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa hadi kwenye masoko mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Tanga.

Vilevile, Mhandisi Msama ameeleza kuwa Tanroads Mkoa wa Tanga inaendelea kutekeleza miradi mitatu ya dharura iliyosababishwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya, kwa gharama ya Sh11.27 bilioni.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Msangazi lenye urefu wa mita 30 lililopo katika barabara ya Amani – Muheza, kilomita mbili kutoka barabara kuu ya Tanga – Segera, kwa gharama ya Sh4 bilioni,  ujenzi wa boksi daraja la Bwiko lenye urefu wa mita 16.5 na barabara unganishi zenye urefu wa mita 630, litakalogharimu Sh3 bilioni na ujenzi wa Daraja la Sagasa lenye urefu wa mita 39 katika barabara ya Kwaluguru – Kiberashi, litakalogharimu Sh4.1 bilioni.