Ibenge aona kitu Azam, awaonya mapema mastaa wake

KATIKA misimu 10 ya ushiriki wa michuano ya kimataifa iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Azam FC haijawahi kufuzu hatua ya makundi hali inayomfanya kocha wa kikosi hicho, Florent Ibengé kuzicheza kwa akili mechi mbili zijazo ili kuweka rekodi mpya. Huu ni msimu wa 11 kushiriki CAF.

Mechi hizo ni dhidi ya KMKM ya Zanzibar ambapo ya kwanza ni Jumamosi wiki hii Oktoba 18, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kisha marudiano Oktoba 24, 2025, Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Katika kuhakikisha inaanza vizuri ugenini, Jumatatu ya Oktoba 13, 2025 kikosi cha Azam kiliekea Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi hiyo ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Licha ya wadau wengi kuona Azam ina kibarua chepesi kwa kukabiliana na kikosi cha Mabaharia hao, kwa Ibenge ni tofauti na amewachimba mkwara mastaa wa kikosi hicho kutowachukulia poa wapinzani wao.

“Nimewaambia wachezaji wangu wazi, hakuna mchezo rahisi katika mashindano ya CAF. Timu yoyote inayofika hatua hii ina ubora. Tusipokuwa makini, tutajikuta tunapata matokeo yasiyotabirika,” amesema Ibengé.

IBE 03

Kocha huyo raia wa DR Congo, amesema amefuatilia rekodi za KMKM na kugundua ina nidhamu ya kiufundi na wachezaji wanaocheza kwa bidii.

“Hawa si wachezaji wa kubahatisha. Wanajua wanachotaka, wanacheza kwa kujituma, hasa wanapokuwa nyumbani. Tunapaswa kuwa tayari na ndio maana tukaona kuna haja ya kuja mapema Zanzibar,” ameongeza.

IBE 01

Azam imefika Zanzibar ikiwa na wachezaji pungufu kutokana na wengine kama Feisal Salum, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Pascal Msindo na Lusajo Mwaikenda kuwa katika majukumu ya timu za taifa katika kipindi cha kalenda ya FIFA.

Hivyo kundi hilo la wachezaji wengine linatarajiwa kuwasili Alhamisi visiwani humo baada ya kutoka Dubai ambako Taifa Stars leo Oktoba 14, 2025 imecheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Iran.

Azam imetinga hatua hii ya pili kufuatia kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 4-0 dhidi ya El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini, huku KMKM ikiing’oa AS Port ya Djibout kwa jumla ya mabao 4-2.

Kwa mujibu wa rekodi, Azam imefungwa katika mechi mbili za mwisho dhidi ya KMKM zote ikiwa katika mashindano ya Cecafa Kagame, 2021, ilianza kuchapwa kwa mabao 3-2 kabla ya bao 1-0.

Rekodi zinaonyesha kwamba, matajiri wa Chamazi, Azam, tangu imeanza kushiriki mashindano ya Afrika haijawahi kufika hata makundi.

IBE 02

Huu ukiwa ni mwaka wa 21 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo 2004, Azam imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili, 2015 ilipotolewa hatua ya awali na Al Merrikh ya Sudan, kisha msimu uliopita 2024-2025 ikatolewa tena hatua ya kwanza na APR.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, imeshiriki mara nane, ya kwanza ikiwa 2013, iliondoshwa hatua ya kwanza na Barrack Young Controllers ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya hatua ya awali kuichakaza El Nasir ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1.

MATOKEO YA AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO

Azam 8–1 El Nasir (hatua ya awali)

Barrack Young Controllers 1–2 Azam (hatua ya kwanza)

Azam 1–2 Ferroviário da Beira (hatua ya awali)

Bidvest Wits 3–7 Azam (hatua ya kwanza)

Azam 2–4 Espérance (hatua ya pili)

Azam 1–3 Mbabane Swallows (hatua ya kwanza)

Fasil Kenema 2–3 Azam (hatua ya awali)

Azam 0–2 Triangle United (hatua ya kwanza)

Azam 4–1 Horseed (hatua ya kwanza)

Azam 0–1 Pyramids (hatua ya pili)

Al Akhdar 3–2 Azam (hatua ya pili)

Bahir Dar Kenema 3–3 Azam (penalti 4–3) hatua ya kwanza

MATOKEO YA AZAM LIGI YA MABINGWA 2015

Azam 2–3 Al-Merrikh (hatua ya awali)

Azam 1–2 APR (hatua ya kwanza)