Mambo sita pekee yanayoutofautisha uchaguzi mkuu wa 2025 na zingine

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025 unaandika kihistoria mpya inayoutofautisha na chaguzi zilizopita. Uchaguzi huu wa saba tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini, unahusisha vyama 17 vilivyosimamisha wagombea urais.

Sura ya upinzani, sheria mpya ya uchaguzi, ushiriki wa kijamii, muundo wa kampeni na ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu ni mambo yanayojenga historia mpya ya uchaguzi Tanzania tangu uhuru wa Taifa.

Hali hii ya kisiasa iliyotangulia uchaguzi huu, kila hatua ya mchakato imekuwa na mambo mapya kuanzia kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) hadi uendeshaji wa kampeni, imeibua mjadala wa kipekee.

Wachambuzi wa siasa wanasema hali hii inaashiria mabadiliko katika mfumo wa kisiasa, kisheria na kijamii, wakiibua mjadala kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini.

Uchaguzi bila vyama vikuu

Mojawapo ya tofauti kuu za uchaguzi huu ni kukosekana kwa vyama vikuu vya upinzani. Kwa mara ya kwanza tangu uhuru, Tanzania inashiriki uchaguzi mkuu huku vyama vikuu vya upinzani; Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo vikiwa nje ya kinyang’anyiro hicho kwa sababu tofauti.

Chadema hakishiriki uchaguzi huu kutokana na msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi kikishinikiza mageuzi ya sheria za uchaguzi na mabadiliko katika muundo wa Tume ya Uchaguzi kupitia kaulimbiu yake ya No reforms, No Election.

ACT-Wazalendo kikikosekana kwenye kinyang’anyiro cha urais baada ya mgombea wake wa kiti hicho, Luhaga Mpina, aliyehamia kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwa katika mkwamo wa kisheria, kesi ambayo bado inaendelea mahakamani.

Akizungumza na Mwananchi, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Profesa Mohammed Makame anataja ukosefu wa maandalizi ndani ya vyama vya upinzani kuwa ni moja ya sababu za baadhi ya vyama kutoshiriki uchaguzi mkuu akirejea mfano wa Zanzaibar katika chaguzi za nyuma.

“Kwa Zanzibar, ilishawahi kutokea uchaguzi mkuu bila vyama vikuu vya upinzani, kwa bara ni jambo jipya. Kukosekana muunganiko miongoni mwa wanachama na maandalizi ya mapema ya wagombea ndani ya vyama vya upinzani ni moja ya sababu vyama hivyo kukosa ushiriki.

“Kama chama kinaandaa mgombea dakika za mwisho wa uteuzi, inaashiria hakina maandalizi na lengo la mgombea wa sifa zipi wanamhitaji,” anasema Profesa Makame.

Hali hiyo imekifanya CCM kushindana na vyama vidogo katika hali inayodaiwa na wachambuzi kuwa imeshusha ushindani kwa chama hicho tawala kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, tofauti na historia ya chaguzi za awali zilizoshuhudia shamrashamra za ushindani wa CCM na vyama vikuu vya upinzani.

Uchaguzi wa 2025 unaendeshwa kwa kutumia sheria mpya za mwaka 2024, ambazo ziliibua mabadiliko ya kisheria. Bunge lilipitisha sheria mpya tatu ambazo ni Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya 2024.

Sheria hiyo imeifanyia mabadiliko iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuanzisha INEC, taasisi ambayo upatikanaji wa mwenyekiti na wajumbe wake umebadilika tofauti na ilivyokuwa awali.

Sheria nyingine zilizopitishwa na Bunge ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo imefanyiwa mabadiliko ili kukidhi mahitaji ya sasa ambayo yamekuwa yakipiganiwa na vyama vya siasa.

Hali hiyo inafanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa wa kipekee ukilinganisha na chaguzi zilizopita ambapo wadau wa uchaguzi walikuwa na malalamiko mengi ambayo mengi yamefanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa katika muundo wa Tume hii mpya.

Ushiriki mkubwa wa wanawake

Tofauti na chaguzi nyingine zilizopita katika historia ya Tanzania, uchaguzi huu umeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wanaogombea nafasi za juu za kisiasa, ikiwamo urais na umakamu wa Rais.

Hali hii inatajwa kama ishara ya maendeleo katika usawa wa kijinsia, tofauti na chaguzi zilizopita ambapo ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu haukuwahi kuifikia kiwango hiki.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wanawake watatu wanagombea urais, ambao ni Samia (CCM), Mwajuma Noty Mirambo (UMD) na Saum Hussein Rashidi (UDP) huku vyama 10 vikisimamisha wanawake katika nafasi ya umakamu wa rais kama wagombea wenza.

Aidha, jumla ya wanawake 558, sawa na asilimia 32 ya wagombea wote 1,735 wa ubunge wa majimbo, wanashiriki uchaguzi wakiwania nafasi hiyo. Hii ni mara ya kwanza kushuhudia idadi hiyo kubwa ya wanawake kushiriki kugombea nafasi za juu za uongozi nchini.

CCM, kinachopewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huu, kwa mara ya kwanza katika historia yake, kimesimamisha mgombea urais mwanamke, Samia Suluhu Hassan, anayetetea kiti hicho baada ya kukikalia kufuatia kifo cha mtangulizi wake, hayati John Magufuli, Machi 17, 2021.

Profesa Makame anataja juhudi za taasisi za kimataifa na hamasa ambayo imekuwa ikifanywa na wadau mbalimbali nchini kuwa moja ya sababu ya ushiriki mkubwa wa wanawake katika siasa, akisisitiza hatua kuendelea kuchukuliwa kufikia lengo la kuwa na asilimia 50 ya wanawake katika nafasi za uongozi wa umma.

“Kuhusu ushiriki huu mkubwa wa wanawake, ni matokeo ya msukumo wa dunia katika kujenga uelewa wao kushiriki katika nafasi za uamuzi.

“Hii inaashiria hatua za ndani pia zimechukuliwa na kuleta matunda juu ya hilo, hata hivyo bado hatujafikia kiwango tulichojiwekea kama taifa kufikia asilimia 50 ya wanawake kwenye nafasi za uongozi wa umma,” anasema mwanazuoni huyo.

Kampeni nyumba kwa nyumba

Mchakato wa kampeni za uchaguzi wa mwaka huu umeonyesha mabadiliko ya kipekee. Mikutano ya hadhara imepungua kwa kiasi kikubwa huku kampeni za vyama vingi zikihamia chini kwenye ngazi ya mtaani na nyumba kwa nyumba.

Njia hii imeonyesha mabadiliko ya uendeshaji wa kampeni, ikiwapa wagombea nafasi ya kuwasiliana moja kwa moja na wapigakura wao ikiwemo kuzungumza na kupeana namba za simu.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anataja gharama za uendeshaji wa mikutano kuwa sababu ya wagombea kutumikia njia hii.

“Kuandaa mkutano wa hadhara ni gharama kubwa, hivyo wagombea wengi hasa hawa wa vyama vidogo hawawezi kumudu gharama hizo ndiyo maana wengi wanakimbilia kampeni za kukutana mtu mmoja mmoja ili kupunguza gharama,” anasema.

Hali hiyo inatofautisha uchaguzi huu na chaguzi zilizopita ambapo mikutano ya hadhara ilikuwa njia kuu ya kuwasiliana na wapigakura, hata hivyo wataalamu wa siasa wanaona njia hii inaashiria kukosekana kwa wagombea wenye ushawishi na kupunguza nguvu ya mshikamano wa chama cha siasa kama taasisi kwenye majukwaa ya siasa.

Uchaguzi wa 2025 umeibua nguvu kubwa ya kushiriki, kusikika na kufuatiliwa kwa vyama vidogo ambavyo vimepata nafasi kubwa zaidi ya kushiriki na kuonyesha sauti zao.

Vyama vidogo ambavyo awali havikuwa na sauti katika siasa za kitaifa, mwaka huu vimeibuka na kupata nafasi ya kujipambanua huku wananchi wakivifuatilia na kuchambua sera zake zinazoenezwa na wagombea wake hasa kwa nafasi ya urais.

Dk Mbunda anataja kukosekana kwa vyama vikuu vya upinzani kama fursa iliyotoa nafasi hiyo kwa vyama vidogo kusikika na kupata wafuatiliaji, akidokeza kushuka kwa ari ya ushindani na shamrashamra za wafuasi wa vyama kutokana na vyama vyao kukosa wagombea.

“Uchaguzi umepoa sana kwa kukosa mambo mengi haasa kukosekana kwa ushindani na upinzani wenye nguvu, hivyo wananchi wamehamia kufuatilia vyama hivi vidogo vinavyoshiriki kwa kukosa wagombea wa vyama vikubwa,” anasema.

Hii ni tofauti kabisa katika historia ya chaguzi zilizopita, ambapo vyama vidogo hata viliposhiriki uchaguzi havikuwa vikisikika kama ilivyo mwaka huu.

Mara nyingi vilifunikwa na majina ya vyama vikuu vya upinzani katika mijadala ya uchaguzi, ambapo kukosekana kwa vyama vikuu hivyo katika uchaguzi huu imekuwa fursa kwa vyama vidogo kushiriki kwa wingi na kusikika zaidi.

Katika mwendelezo wa sura mpya ya uchaguzi wa mwaka huu, wagombea wengi wameahidi kuleta mageuzi ya haraka ndani ya siku 100 za kwanza madarakani.

Mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuanzisha Tume ya Maridhiano na Upatanishi ndani ya siku 100 za kwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuleta umoja na kuimarisha utawala bora.

Wakati huohuo, Salum Mwalimu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) akiahidi mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100 za kwanza.

Mgombea urais wa Chama cha AAFP, Kunje Ngombare Mwiru ameahidi kujenga bwawa maalumu lenye mamba Ikulu kwa ajili ya kuwachukulia hatua mafisadi ikiwa ni njia ya kukabiliana na ufisadi.

Profesa Makame anataja mabadiliko ya mifumo ya siasa nchini kutokana na kukua kwa uelewa wa Watanzania kuwa kichocheo cha mabadiliko ya mbinu za kisiasa katika demokrasia inayoendelea kukua nchini.

“Uelewa wa Watanzania unaendelea kubadilika, hatua hii inabadili pia mbinu za kisiasa kutoka kuwaita na kuwakusanya watu kuwahubiria kwenda kwenye siasa za mazungumzo moja kwa moja kati ya watu na wagombea, hii inawezekana ikawa njia sahihi kwani kumshirikisha mtu kwa ukaribu inajenga imani zaidi,” amesema na kuongeza:

“Tofauti na zamani, siku hizi vyama vinazungumzia kura kwa kuchambua idadi ya wanachama wao, vinaangalia pia idadi ya Watanzania kwa ujumla na idadi ya waliojiandikisha kupiga kura, hivyo kampeni ya nyumba kwa nyumba huenda ni mbinu sahihi kuwafikia watu wao moja kwa moja tofauti na kuhutubia mkutano wa kiujumla jukwaani,” amesema.

Dk Mbunda, anadokeza kuwa mabadiliko yalioonekana katika uchaguzi huu yanapaswa kuangaliwa katika mustakhabali wa maendeleo ya demokrasia na chaguzi zijazo nchini ili kuhakikisha dosari zilizopo zinashughulikiwa na kuwa na chaguzi zinazoshirikisha vyama vyote.