Dar es Salaam. Kipindi rasmi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kilianza Agosti 28, 2025 na kinatarajiwa kumalizika Oktoba 28, 2025 kikiashiria miezi miwili ya shughuli nyingi za kisiasa kote nchini.
Kutoka mitaa yenye pilikapilika ya mijini hadi vijijini bado hali ni tulivu, wagombea na wafuasi wao wamekuwa wakizunguka nyumba kwa nyumba wakizungumza moja kwa moja na wananchi mmoja mmoja au vikundi ili kuwashawishi wawapigie kura.
Mbinu hii ya kampeni imesifiwa kwa kuleta siasa karibu zaidi na wananchi, lakini pia imeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa viashiria vya rushwa na mienendo isiyo ya kimaadili, hasa inapotekelezwa katika mazingira ya faragha.
Mkurugenzi wa Kuzuia Rushwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sabina Seja, akizungumza na Mwananchi kuhusiana na hili, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kupitia maeneo matatu muhimu.
Moja amesema ni kutoa elimu kwa umma, kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wanaobainika kujihusisha na rushwa.
Amefafanua kuwa Takukuru inatekeleza jukumu lake la kisheria kwa njia tatu kuu, kwanza, kwa kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya rushwa; pili, kwa kufanya uchunguzi wa kina na tatu, kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa.
Kuhusu kampeni za nyumba kwa nyumba, Sabina amesema hakuna utaratibu wa kisheria unaozielekeza moja kwa moja, hivyo taasisi hiyo haiwezi kuzuia mtu kumtembelea mwingine nyumbani kwake kwa sababu tu ni mgombea.
Hata hivyo, ameongeza kuwa hali hiyo inafanya iwe vigumu kufahamu kinachoendelea katika mazungumzo hayo ya faragha.
“Hatuna uwezo wa kuzuia watu kutembeleana, lakini tunasisitiza wananchi wajiepushe na rushwa kwa sababu ni kosa la kisheria na kinyume na maadili ya taifa,” anasema Sabina. Ameongeza kuwa Takukuru inaendelea kutoa elimu kupitia matangazo, ujumbe mfupi wa maandishi na kampeni za uhamasishaji.
Kwa upande wa vyama vya siasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kampeni za nyumba kwa nyumba ni njia ya kuwafikia wananchi moja kwa moja na kueleza sera zake. Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Bara, John Mongella amesema chama hicho kina mtandao mpana wa wanachama unaokifanya kuendesha kampeni zake kwa hoja, badala ya vishawishi vya kifedha.
Mongella amesisitiza kuwa wanachama wa CCM wanakumbushwa kila mara kuepuka kutoa fedha au zawadi kwa wapiga kura kwa sababu ni kinyume na maadili ya chama chao.
“Njia yetu inalenga kusikiliza wananchi na kuelewa changamoto zao, si kuwahonga. Tunataka kushinda kwa hoja, si kwa fedha,” amesema Mongella.
Kwa upande wa ACT-Wazalendo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema mbinu hiyo inawawezesha wagombea kuwasiliana moja kwa moja na wapigakura kwa namna ambayo mikutano ya hadhara mara nyingi inashindwa kufanyika.
Ado amesema mikutano mikubwa huvutia watu wengi, lakini si wote wanaohudhuria kwa nia ya kusikiliza sera.
“Wapo wanaokuja kwa ajili ya muziki au burudani, lakini unapomtembelea mtu nyumbani kwake, unapata muda wake wote na kujenga mazungumzo ya kweli,” amesema.
Amekanusha madai kuwa mbinu hiyo inaweza ikashawishi wagombea kutoa rushwa akisisitiza kuwa chama chake kimejikita katika siasa safi. “Nguvu yetu ipo katika hoja, si katika fedha. Tunawaelekeza wanachama wetu kushinda kwa hoja, si kwa bahasha,” amesema.
Chama cha Wananchi (CUF) nacho kimeeleza kuwa kampeni za nyumba kwa nyumba ni muhimu hasa kwa vyama vidogo vyenye rasilimali chache.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya amesema uwanja wa siasa mara nyingi hauko sawa, hivyo vyama vidogo hulazimika kutumia njia hii ili kuwafikia wapiga kura ambao vinginevyo wanaachwa nyuma.
Amesema mikutano mikubwa inawafaidisha zaidi wenye uwezo wa kifedha na upatikanaji wa vyombo vya habari, lakini kwa CUF, kampeni za nyumba kwa nyumba ni njia ya kuendelea kuonekana na kueleza sera zake.
Hata hivyo, amekiri kuwa mbinu hiyo inaweza kutumika vibaya endapo mawakala hawatakuwa waadilifu.
Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Joseph Selasini, amesema kampeni hizo ni njia ya kurejesha imani kati ya wananchi na wanasiasa. “Wananchi wamechoshwa na siasa za majukwaani. Wanataka viongozi wanaowasikiliza moja kwa moja majumbani mwao,” amesema.
Selasini amesisitiza kuwa chama chake kimewaelekeza wagombea wake kuepuka tabia zozote zinazoweza kuchukuliwa kama rushwa. “Tunataka kuonyesha kuwa siasa ya kujenga uhusiano haihitaji fedha,” ameongeza.
Wachambuzi wa siasa wanasema mbinu ya nyumba kwa nyumba ni yenye nguvu lakini pia hatarishi.
Profesa Makame Ali Ussi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), amesema ukaribu wa mazungumzo ya nyumbani unaweza kujenga uaminifu, lakini pia kuficha mambo yasiyo ya kimaadili.
“Mgombea anapokaa nyumbani kwako na kuzungumza lugha yako, unamsikiliza kwa makini, lakini faragha hiyo hiyo inaweza kuficha vitendo vya rushwa,” amesema.
Ameongeza kuwa katika mila za Watanzania, kutoa zawadi kama sukari au mafuta huonekana kama upole, lakini katika kipindi cha kampeni, vitendo hivyo vinaweza kutafsiriwa kama rushwa.
Dk Onesmo Kyauke wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alieleza kuwa kampeni za nyumba kwa nyumba ni upanga wenye makali mawili unaoweza kusaidia vyama vidogo lakini pia huongeza hatari ya tuhuma.
“Ni mbinu nzuri kwa wasioweza kufanya mikutano mikubwa, lakini inaweza kutafsiriwa vibaya ikiwa kutatokea utoaji wa zawadi,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Paul Loisulie wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema kuongezeka kwa kampeni za aina hiyo ni dalili ya ukuaji wa demokrasia ya Tanzania, inayojenga mawasiliano ya moja kwa moja badala ya maonyesho makubwa.
“Tunaingia kwenye zama mpya za siasa za mazungumzo. Ni mwelekeo chanya, lakini unahitaji uwajibikaji mkubwa. Mkono wa salamu usifuatiwe na bahasha,” amesema Dk Loisulie.