Chama cha ACT – Wazalendo kimetoa Ilani ya Uchaguzi kwa Zanzibar, ikibainisha msimamo wake kuhusu mamlaka kamili, masuala ya Muungano na mwelekeo wa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ilani hiyo inayohusu uchaguzi wa Oktoba 28 na 29 mwaka huu kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi, huku Katiba ikieleza uchaguzi wa Rais wa Zanzibar kufanyika siku moja, imetayarishwa na wataalamu wa masuala ya uchumi, elimu, afya, sheria, ustawi wa jamii na walimu.
Wataalamu hao ni Watanzania kutoka Bara na Visiwani wakiwamo wazaliwa wa Zanzibar wanaofanya kazi katika nchi za Ghuba, Canada, Ulaya, India, Australia na Marekani.
ACT – Wazalendo pia ina ilani kwa Tanzania Bara yenye msisitizo katika masuala ya Muungano.
Katika uzinduzi wa ilani hiyo, Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman ambaye ni mgombea urais wa chama hicho Zanzibar, alisema wanapozungumzia mamlaka kamili hawakusudii kudhoofisha Muungano bali kuuimarisha.
Alifafanua kuwa lengo la chama hicho ni kuwawezesha Wazanzibari kujiamulia mambo yao yenye maslahi kwao bila kuathiri Muungano, jambo analosema linaweza kufikiwa kupitia mazungumzo ya kweli yanayoangalia hali halisi, badala ya misukumo ya kisiasa. Kwa mujibu wa ACT – Wazalendo, kinachotakiwa ni kuhakikisha hakuna mshirika wa Muungano anayelalamika kwa kurejea mkataba wa Muungano wa mwaka 1964 uliotaja wazi mambo ya Muungano.
Kauli hiyo imekuja huku wapinzani wao wakuu Chama cha Mapinduzi (CCM) wakidai kuwa dhamira ya ACT – Wazalendo ni kuvunja Muungano. Hata hivyo, inashangaza kuona baadhi ya wanaoishutumu ACT – Wazalendo ndio waliosikika mara kadhaa ndani ya Baraza la Wawakilishi wakilalamikia Muungano huo.
Kumbukumbu za BLW zinaonyesha kuwa walidai Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ifunge virago na kuondoa baadhi ya taasisi za Muungano, hasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ninachojiuliza, kwa nini leo wanatoa kauli tofauti na zile za awali? Kwa sababu ACT – Wazalendo kinasisitiza kuwa kikipewa ridhaa, kipaumbele kitakuwa kurejesha thamani ya utu visiwani na kuzuia watu wasiokuwa na hatia kuumizwa au kuuawa kwa sababu ya kutaka kushika hatamu za uongozi.
Othman nilimsikia akisema chama chake kitaendelea kuheshimu Katiba na hakitaruhusu kutungwa kwa sheria zinazokwenda kinyume nayo, kama inavyofanyika sasa.
Tena akasema chama hicho kinakusudia kuandika Katiba mpya itakayohakikisha hakuna mtu aliye juu ya sheria na kila anayevunja sheria atawajibishwa bila kujali wadhifa wake.
Vilevile, chama hicho kimeahidi kutokuwa na uvumilivu dhidi ya uvunjaji wa haki za binadamu, rushwa na ufisadi.
Katika mapambano dhidi ya uovu huo, ilani ya ACT – Wazalendo imeweka msisitizo wa kuchukua hatua za vitendo badala ya kutoa kauli au maandishi ya kujisifia.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, ufisadi Zanzibar umeota mizizi katika miradi mikubwa inayotolewa kwa makandarasi kinyemela bila zabuni za wazi, huku gharama zikiwa juu kuliko thamani halisi.
Kuhusu ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi, kimeeleza kuwa kikishika madaraka, hakitakuwa chama tawala bali chama kinachoongoza utawala; wananchi ndio watakuwa wenye mamlaka, na Serikali haitatoa amri au kufanya maamuzi yasiyo na tija kwa umma. Kwa mtazamo wa ACT – Wazalendo, Wazanzibari kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ongezeko la kodi na matumizi mabaya ya mapato ya serikali.
Hivyo, hatua ya kwanza itakayochukuliwa ni kupunguza viwango vya kodi, ikiwamo ile ya petroli ambayo ni kubwa kuliko bei ya Dar es Salaam. Chama hicho pia kimepanga kupitia upya mikataba ya serikali ili kufunga mianya ya rushwa na kuhakikisha ufuatiliaji sahihi wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, ili kuzuia mtu mmoja au kikundi kidogo kuwa na mamlaka makubwa.
Katika mfumo wa manunuzi, kila Mtanzania atapewa nafasi sawa kushiriki katika ushindani, huku wazalendo wakipewa kipaumbele. ACT – Wazalendo pia inakusudia kushirikisha sekta binafsi kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, lakini haitabinafsisha taasisi nyeti kama bandari, viwanja vya ndege, elimu na afya.
Kwa upande wa Wazanzibari na Watanzania wa Diaspora, kimeahidi kuwapa haki sawa na wale walioko nchini, ikiwamo kumiliki ardhi, kupiga kura na kugombea nafasi za uongozi, kwa hoja kwamba huwezi kumtaka mtu awe mzalendo wakati humpi haki zake.
Katika mikutano yake ya kampeni, kimetoa takwimu kuhusu vitendo vya udikteta, ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu na kuahidi kuyakomesha mara itakapopata nafasi ya kuongoza Zanzibar.
Kwa sasa, vyama vyote vya siasa vinaendelea na kampeni; ingawa siasa za chuki na matusi zimepungua ukilinganisha na chaguzi zilizopita, tuendelee kumuomba Mola aiweke Zanzibar katika amani, uchaguzi upite salama, amani iendelee kutamalaki na siyo mtihani mwingine wa maafa.