Watanzania Wakumbuka Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere – Video – Global Publishers


Oktoba 14, 2025 — ni kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyeaga dunia Oktoba 14, 1999, katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London, Uingereza.

Katika kuadhimisha siku hii muhimu, Global TV imetembelea eneo la Magomeni, jijini Dar es Salaam, ambako Mwalimu Nyerere aliwahi kuishi na familia yake katika miaka ya 1950, kipindi ambacho alikuwa mstari wa mbele katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Grace Buberwa, ambaye ni miongoni mwa majirani waliowahi kuishi mtaa mmoja na Hayati Nyerere, ameelezea kwa hisia jinsi maisha yalivyokuwa wakati huo.

“Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa kawaida sana, mwenye upendo na heshima kwa kila mtu. Tulimwona akipita akienda kazini au kwenye mikutano ya TANU bila ulinzi wala majivuno. Tulijifunza unyenyekevu kutoka kwake,” amesema Grace.

Maeneo mengi nchini yameendelea kufanya shughuli za kumbukizi, ikiwemo ibada, dua na midahalo ya kuenzi falsafa na maadili aliyoyaacha Mwalimu Nyerere, ikiwemo umoja, uzalendo na utu.

Mwalimu Nyerere anakumbukwa kama kiongozi aliyesimamia uhuru, umoja wa kitaifa na maendeleo ya kijamii, na mchango wake unaendelea kuwa dira kwa viongozi wa sasa na vizazi vijavyo.