WANUFAIKA wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) mkoani Tabora wametakiwa kutumia fedha za ruzuku walizopewa kwa kufuata masharti ili kuhakikisha malengo ya kuboresha maisha ya wananchi na kuhifadhi misitu yanafikiwa.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dkt. Tuli Msuya, ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo kwa vikundi zaidi ya 10 vya wafugaji nyuki vilivyonufaika na ruzuku kutoka mfuko huo.
Amesema fedha hizo ni mali ya umma na zinapaswa kugharamia miradi yenye tija kwa jamii hasa inayochangia uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za misitu nchini.
Dkt. Tuli amesema fedha za ruzuku zimetolewa ili ziwe kichocheo cha maendeleo na uhifadhi endelevu wa misitu, hivyo ni lazima zitumike kwa kuzingatia masharti ya mkataba wa utoaji fedha hizo na kusisitiza TaFF haitavumilia matumizi yasiyo na tija.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 14 ya uendeshaji wake, TaFF imetumia Sh. bilioni 57.5 kugharamia miradi 1,245 nchi nzima, ambapo kati ya hizo, Sh. bilioni 3.1 zimetumika kutekeleza miradi 74 katika wilaya saba za Mkoa wa Tabora.
Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa jengo la mihadhara katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki (BTI) pamoja na viwanda vitatu vya kuchakata mazao ya nyuki vilivyopo Tabora, Sikonge na Nzega, ambavyo vinatarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya nyuki na kukuza kipato cha wananchi.
Kwa upande wake, Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka TaFF, John Malemo, amewataka wanufaika kuhakikisha wanaandaa na kuwasilisha taarifa za matumizi ya fedha kwa wakati ili kurahisisha utoaji wa fedha za awamu zinazofuata, akisisitiza kuwa uwazi na uwajibikaji ndio msingi wa uendelevu wa ruzuku hizo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TaFF kwa kuwajengea uwezo, wakiahidi kutumia mafunzo hayo kuboresha shughuli za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali, hatua ambayo wamesema itasaidia kuufanya Mkoa wa Tabora kuwa kinara wa uzalishaji wa asali nchini.