Unguja. Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema katika Serikali ijayo, atahakikisha inazingatia na kuweka usawa kila sekta kuzingatia watu wenye ulemavu huku akiahidi kuwapa kipaumbele kwenye nafasi zake 10 za uteuzi.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 15, 2025 wakati akizungumza na watu wenye ulemavu katika Ukumbi wa Idrissa Abduwakil, ikiwa ni sehemu ya kampeni za chama hicho ambacho kimekuwa na utaratibu wa kupiga kampeni na kuomba kura kwa kukutana na makundi mbalilbali.
“Tutahakikisha tupo pamoja na watu wenye ulemavu ili kuondoa changamoto zinazowakabili, kwa hiyo tunaomba mtupe ridhaa nyingine tuendelee kutekeleza mazuri tunayopanga na nyie ni mashahidi tukiahidi tunatekeleza hakuna sababu ya kutotupigia kura,” amesema Dk Mwinyi.

Zahara Makame Said akimweleza mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinnyi changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu wakati akizungumza na makundi hayo katika ukumbi wa Idrissa Abduwakil ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuomba kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika kuleta usawa amesema atahakikisha katika vyombo vya kutunga sheria wanaongezwa watu wenye ulemavu na kutoa kipaumbele kwenye ajira zingine za Serikali ambazo kwa namna moja ama nyingine itasaidia kwa ukaribu kusikilizwa changamoto zao.
Amesema watajega kituo maalumu chenye vifaa saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu ili kuwasaidia kupata vifaa muhimu kwa ajili ya huduma zao bila gharama zozote.
Pamoja na kujenga kituo hicho, amesema wataondoa ushuru wa vifaa vya watu wenye ulemavu ili vipatikane kwa urahisi.
Kwa upande wa miundombinu ya hospitali, Dk Mwinyi amesema “Katika hospitali zinazojengwa lazima kuzingatia mahitaji muhimu ya watu wenye ulemavu, huduma za tiba katika hospitali zitakuwa na vitengo kwa ajili ya watu wenye ulemavu.”
Kwa upande wa uwezeshaji, mgombea huyo wa urais amesema wataendelea kuwapa mafunzo, mazingira bora ya kufanyia biashara zao kulingana na mahitaji yao huku wakipewa mitaji.
“Haya yote tumeshayaanzisha, lakini tutayaendeleza kwa nguvu zaidi kuhakikisha hakuna.

Awali wakizungumza baadhi ya watu wenye ulemavu wameeleza changamoto wanazokutana nazo wakiomba zifanyiwe kazi Ili kupata fursa sawa kama wanavyopata wengine.
Ali Omar kutoka Shirikisho la Watu wenye Ulemavu, ameomba kijengwe kituo kikuu cha kitaifa cha marekebisho ya watu wenye ulemavu ambacho kitawasaidia katika utoaji wa huduma muhimu badala ya kusafirishwa kwenda nje ya Zanzibar.
“Tukipata hiki kituo cha kitaifa kinaweza kusaidia uzalishaji wa vifaa saidizi na tutakuwa na wataalamu na vifaa vya kutosha,” amesema.
Pia ameomba kuangaliwa utaratibu wa kutoa pensheni jamii kwa watu wenye ulemavu kwani kuna familia ambazo zina watu wenye ulemavu huku akiomba kuangalia namna ya kupunguza umri wa kutoa pensheni jamii kutoka miaka 70 hadi 60 ili kuwasaidia wengi zaidi.
“Anayestaafu kwa miaka 60 hapohapo aingie kwenye pensheni jamii badala ya kusubiria afikishe miaka 70,”
Kadhalika, amesema licha ya hospitali nyingi kujengwa na kuwekewa miundombinu ambayo inazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, bado kuna haja ya kuongeza zaidi miundombinu hiyo kutokana na changamoto nyingi zinazowakumba.

Naye Mboje Abdallah Mussa kutoka Mangapwani amesema watu wenye ulemavu hawapewi kipaumbele akaomba wasingatie hilo.
“Tunaomba tupewe nafasi katika maeneo mbalimbali kulingana na uwezo wetu, mara nyingi hatupewi kipaumbele,” amesema Mboje.
Kwa upande wake Juma Abdalla Yussuf amesema vimejengwa viwanja vingi vya michezo lakini, wanaomba na wao kupewa utaratibu wa kutumia viwanja hivyo.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema ilani ya chama hicho imeeleza namna ambavyo watahakikisha mazingira na upatikanaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu.
“Hata kabla ya kuja hapa, ilani yetu imeshaelekeza namna ambavyo tunatakiwa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika masuala ya ajira, kutoa ruzuku na kutoa vifaa saidizi,” amesema.