Rais Samia Atuma Salamu za Rambirambi Kwa Kifo cha Raila Odinga – Global Publishers



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, kilichotangazwa hivi karibuni.

Kupitia taarifa yake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kiongozi huyo mashuhuri, akimtaja kuwa mwanamajumui wa kweli wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye mchango wake uliivusha Kenya na kugusa Afrika Mashariki na bara zima la Afrika.

Rais Samia amesema msiba huo si wa Kenya pekee bali ni wa Afrika nzima, kutokana na mchango mkubwa wa Odinga katika kuimarisha umoja, amani na demokrasia katika bara hilo.

Aidha, Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Samoei Ruto, pamoja na Mama Ida Odinga, familia, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Kenya, akiwatia moyo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Afrika imepoteza mmoja wa viongozi wake jasiri, mwenye maono na aliyekuwa na dhamira ya dhati ya kuona bara letu linakuwa na umoja, amani na maendeleo endelevu,” amesema Rais Samia.