Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, wanawake wanapojitambua, kujiamini, na kuwa tayari kuwaongoza wengine, hufungua milango ya mabadiliko chanya.
Hayo yamebainika katika mahafali ya nne ya mafunzo ya wanawake katika uongozi, kupitia program ya G for G (Girl for Girl) inayoendeshwa juzi na Kampuni ya Alaf Tanzania jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Lincoln Du Plessis amesema program hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa, mbali na mambo mengine, imewajengea wanawake wa kampuni hiyo kujiamini zaidi katika majukumu yao kazini.
Amewaasa wahitimu wa program hiyo kutambua kuwa, uongozi ni uwajibikaji na sio nafasi tu anayopewa mtu.
“Ni lazima muwe tayari kuwaongoza wengine ili nao wapate maarifa mliyoyapata ninyi na wapate ari ya kuwa viongozi wanaowajibika,” amesema.
Du Plessis pia amewakumbusha wahitimu hao kuhusu kujiamini na kuwa na mawazo chanya ili wawe viongozi bora katika kampuni hiyo.
“Hii ni kama safari ambayo ina milima na mabonde, kwa hiyo lazima mjiandae kukabiliana na yote haya ili muwe viongozi bora,”amesema.
Akifafanua kuhusu mafunzo hayo ya wanawake na uongozi, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Alaf, Hawa Bayumi amesema mafunzo hayo ni ya nne tangu kuanzishwa kwa programu hiyo ambayo imekuwa na manufaa makubwa huku wanawake wengi zaidi wakipata nafasi za uongozi .
“Leo hii wamehitimu wanawake 10 ambao wamepata mafunzo mbalimbali na maarifa yatakayowasaidia katika shughuli zao za kila siku hususani uongozi,” amesema.
Katika mahafali hayo wahitimu hao, kutoka idara mbalimbali walipata vyeti baada ya kupitia mafunzo ya miezi kadhaa ya nadharia na vitendo hivi kuwajengea uwezo zaidi.
“Mimi mwenyewe ni matunda ya program hii na nilikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kabisa kupata mafunzo haya na kuhitimu na sasa hivi nafurahi kuwa mmoja wa viongozi,”amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wote, Pamela Mwanjali ambaye ni Meneja Mauzo Kanda ya Pwani, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa mno kwa kuwa wamehitimu wakiwa watu tofauti na mwanzoni kabla ya mafunzo hayo.
Mwanjali amesema, “kwa niaba ya wenzangu, naishukuru sana Alaf kwa kutujengea uwezo huu na kutuamini kwamba tunaweza kushika nafasi za uongozi. Tumepikwa vizuri na sasa tunakwenda kutekeleza majukumu yetu vizuri zaidi kwa sababu tumejifunza mengi mno.”
Hata hivyo, alitoa wito kwa kampuni zingine na mashirika yawajengee wanawake uwezo ili watambue kuwa na wao wanaweza kuwa viongozi.