Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ameahidi kushughulikia kwa kina changamoto za vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto visiwani humo.
Ahadi hiyo ameitoa leo Jumatano Oktoba 15, 2025 wakati wa kikao chake na maimamu, walimu wa madrasa na masheikh waliotoka majimbo mbalimbali likiwemo la Wingwi, Konde, Tumbe na Micheweni kisiwani Pemba.
Kabla ya kutoa ahadi hiyo, baadhi ya viongozi wa dini walimweleza Othman kuhusu masikitiko yao juu ya kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto jambo linalosababisha kupunguza heshima ya maadili.

Mkazi wa Wingwi, Sheikh Ali Juma Hamad wa Wingwi amesema hivi sasa imekua aibu katika suala la udhalilishaji wa wanawake na watoto katika jamii ya Wazanzibari.
“Unaweza kusikia mzee wa miaka 70 anamuingilia mtoto wa miaka mitano, jamanii hapa ndio tulipofikia ndugu mgombea (Othman) tunapoteza nguvu kazi ya siku za usoni,” amesema Sheikh Hamad.
Kiongozi mwingine, Kombo Khamis Kombo ametilia mkazo suala hilo,akisema ni wakati mwafaka wa kukomesha vitendo vya udhalilishaji kuweka sheria zitakazoondoa changamoto hiyo visiwani humo.
Kwa mujibu wa Takwimu za Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar za zinaeleza jumla ya matukio 97 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa Juni, 2025 Juni, 2025.
Kati ya matukio hayo waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 85.6, wakifuatiwa na wanawake asilimia 12.4 na wanaume asilimia 2.1.
Katika kikao hicho, Othman amesema Zanzibar haiwezi kuwa sehemu ya kuvumilia watenda maovu na kusisitiza kuwa sheria lazima zifuate mkondo wake bila upendeleo.
“Serikali nitakayoiongoza itachukua hatua madhubuti za kupambana na vitendo hivyo ili kulinda haki za wanawake na watoto,”
“Zanzibar imejulikana kama nchi ya visiwa yenye kufuata misingi ya dini, lakini kwa sasa hali imebadilika kutokana na kuongezeka kwa mambo yasiyo na msingi katika jamii,” amesema.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema ni wajibu wa viongozi wa dini, wazazi na walimu kushirikiana katika kuirejesha jamii kwenye maadili mema na misingi ya heshima.
Sambamba na hilo, amesema udhalilishaji umekuwa ukijitokeza katika maeneo tofauti ambayo mara nyingi wanakutana nayo watoto wa kike.

Katika kikao hicho, mgombea huyo ametolea mfano wa ukosefu wa ajira kwa vijana wa kike ni aina nyingine ya udhalilishaji wa kimfumo unaosahaulika na kutopewa uzito unaostahili.
Amefafanua kuwa changamoto hiyo, inawafanya vijana wengi wa kike kuwa katika mazingira hatarishi, jambo linaloweza kuchangia vitendo vya unyanyasaji na ukosefu wa heshima katika jamii.
“Nitalishughulikia kikamilifu suala la ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana wote, hasa kwa wanawake, kwa kuhakikisha kila kijana ana nafasi ya kujiajiri au kupata kazi yenye staha,” ameeleza.
Othman ameahidi kuwa Serikali ya ACT itatengeneza mazingira rafiki ya ujasiriamali, mafunzo ya ufundi na mikopo midogo itakayowezesha vijana kujiendeleza kimaisha, ili kupunguza utegemezi unaochochea udhalilishaji wa kijinsia.
Mbali na hilo, Othman ameahidi kuanzisha mabaraza maalumu ya maadili na usalama wa kijamii katika kila wilaya, yatakayoshughulikia kwa haraka kesi za ukatili wa kijinsia na kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa jamii nzima, hivyo Serikali itakayoundwa na ACT itahakikisha elimu ya kinga na ulinzi wa watoto inatolewa shuleni na kwenye taasisi za dini ili kulinda kizazi kijacho.