HANDENI-TC
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Handeni, mkoani Tanga, Esther Herman, ametoa wito kwa wananchi kuzingatia ulaji wa chakula bora kinachojumuisha makundi sita muhimu ili kuepuka magonjwa yatokanayo na lishe duni.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Chakula Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Tanga, chini ya kaulimbiu “Tuungane pamoja kupata chakula bora kwa maisha bora ya baadaye”, Esther ametaja makundi hayo ni wanga, protini, mboga za majani, matunda, mafuta pamoja na maji.
Amesema kila kundi lina umuhimu wake mwilini, na ulaji usio sahihi unaweza kusababisha udhaifu wa kinga ya mwili, utapiamlo, au uzito uliopitiliza.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa elimu ya lishe kuanzia ngazi ya kaya, akibainisha kuwa jamii nyingi bado hazina uelewa sahihi kuhusu mlo kamili, jambo linalochangia changamoto za afya kwa watoto na watu wazima.