Mbeya. Ubunifu, uwajibikaji mshikamano wa kiutendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, vimetajwa kuwezesha halmashauri hiyo kuibuka kinara kikanda kupitia miradi mitano iliyokaguliwa kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025.
Mwenge wa Uhuru kitaifa uliwasili Mkoa Mbeya Oktoba 7, 2025 ambapo katika Halmashauri ya Mbeya ulikagua miradi mitano yenye thamani ya Sh1.3 bilioni.
Miongoni mwa miradi ni pamoja na ujenzi wa bwalo la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Imezu, Kituo cha kimkakati cha kuzalisha hewa tiba na mingine ikiwa na thamani ya zaidi ya Sh1. 3 bilioni.
Jana Oktoba 14,2025 wakati wa kusoma risala ya utii kwenye kilele cha kuhitimisha mbio hizo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi alitaja halmashauri hiyo kushika nafasi ya kwanza kikanda na kujinyakulia tuzo maalumu.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele hicho ,kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Beno Malisa aliyembatana na Mkuu wa Wilaya Solomon Itunda na Mkurugenzi wa Halmashauri , Erica Yegella.
Ussi amesema mwenge wa Uhuru umeridhishwa na miradi iliyo kaguliwa na hivyo kupelekelea kutoa tuzo maalum kwa kutambua mchango katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Halmashauri hiyo imefanya vizuri katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo hususani katika sekta ya elimu, afya na mikopo asilimia 10 ya vijana wanawake na watu wenye mlemavu.
Akizungumza na Mwananchi Yegella amesema siri kubwa ni kutokana na ushirikiano wa utendaji wa kazi ,uzalendo ,ubunifu na utayari wa kupokea ushauri kwa viongozi wakuu.
“Namshukuru sana Mkuu wa Mkoa na Wilaya ambao walikuwa bega kwa bega kushirikiana nasi katika kila hatua ya utekelezaji na usimamizi wa miradi usiku na mchana mpaka hatua ya kupokea mwenge na hitimisho na hatimaye kuibuka kinara, “amesema Yegella.
Kuhusu ushindi huo,Yegella amesema wamefungua ukurasa mpya wa kuhimarisha mshikamano wa kiutendaji katika kufuatia miradi ya maendeleo ambayo Serikali inaleta fedha sambamba na mapato ya ndani.
“Ushindi ni sehemu ya nyote kung’aa tutaendelea kushirikiana kiutendaji na usimamizi thabiti wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ,lakini niwapongeze watumishi wote kwa ushirikiano na kujituma kwa umoja wetu,” amesema.
Katika hatua nyingine amesema wataendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo lengo ni kuona wanafikia malengo ya Serikali kufikisha huduma muhimu katika jamii .

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Beno Malisa (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Makamu wa Rais ,Philipo Mpango jana Oktoba 14,mwaka huu ,mara baada ya kuhitimisha kilele cha Mbio za Mwenge kitaifa 2025 mkoani hapa.Picha na Hawa Mathias
Kauli za wananchi
Johari Issa amesema hatua hiyo ni matokeo makubwa ya utendaji mzuri wa viongozi wa Mkoa kwa kutanguliza hofu ya Mungu na kutumia vyema fedha za kodi za Watanzania.
“Mwanamke akiwezeshwa anaweza tunajionea kwa vitendo huyo Mkurugenzi ni mwanamke alivyoweza simama kidete matumizi ya fedha za miradi na kupelekea mwenge wa uhuru kutoa tuzo jambo ambalo limeleta heshima kwa Mkoa,”amesema.