Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi ameahidi iwapo atapata ridhaa ya kuongoza dola, Serikali yake itatunga sheria kali kuwabana wanaume wanaotelekeza watoto bila.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 15, 2025 wakati akizungumza na makundi ya wajane, marasta na Jamii ya Ismailia na Hindu katika ukumbi wa Idrissa Abduwakili Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Tutakuwa na sheria kali kuwabana wanaotelekeza watoto, lazima huduma za malezi kwa watoto zisimamiwe na wazazi wote wanaotelekeza watapaswa kubanwa watekeleze wajibu wao,” amesema Dk Mwinyi
Dk Mwinyi amesema anashangaa kuona kuna viongozi wakubwa wanahubiri ubaguzi ilhali jamii za Zanzibar ni mchanganyiko wa watu tofauti.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi Akizungumza na Wajane, marasta, Ismailia na Wahindu katika kampeni za chama hicho ukimbi wa Idrissa Abduwakil Mkoa wa Mjini Magharibi
Amesema chama hicho pekee ndio kinahubiri umoja, mshikamano na kuondoa ubaguzi wa watu kwani wote ni kitu kimoja.
“Ninawashangaa, kuna viongozi wakubwa wanahubiri ubaguzi, lakini ndugu zangu Zanzibar hii kuna mchanganyiko mkubwa wa watu, kuna wenye asili ya Tanzania bara, wenye asili ya Kenya, Wangazija, Waarabu na wa kutoka India.”
“Lakini hawa wote ni Wazanzibari, wanatambulika na kuheshimika, ila kuna wenzetu wamekuwa wakihubiri ubaguzi, sisi watu wote ni wamoja,”
Mgombea huyo amesema kama wanataka amani na maendeleo basi hakuna chama kingine mbadala wa CCM kwani ndio pekee kimeonesha hayo kwa vitendo.
Akizungumza kuhusu uwezeshaji, Dk Mwinyi amesema wataendelea kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapa mikopo na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao.

Awali Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wajane, Tabia Makame amesema kuna wanaume wengi wanawatelekeza watoto hususan kisiwani Pemba jambo ambalo linaongeza mzigo kwa wanawake.
Amesema kwa sasa wapo kwenye mpango kutengeneza kanzi data kubaini wanawake waliotelekezewa watoto, lakini kwa taarifa za awali hali ni mbaya.
“Tena hawa wanawake waliotelekezewa watoto bado ni wadogo kuanzia miaka 18 na kuendelea, changamoto pia inaonekana kwa wazazi kuwaozesha wakiwa bado wadogo,” amesema Tabia.