Fikiria unapanda daladala bila kuhangaika kutafuta chenji, bila wasiwasi kama konda amekurudishia pesa yako au la, wala hofu ya kukabidhiwa noti bandia. Hakuna foleni ya kulipa, na safari inaendelea kwa utulivu bila usumbufu. Malipo yanafanyika papo hapo kwa njia ya kidijitali haraka, salama, na kwa uwazi. Ni ndoto lakini inayoweza kufikiwa kama mustakabali katika kuboresha mfumo wa usafiri maeneo ya miji.
Usafiri wa mijini, kama tunavyojua, bado unategemea malipo kwa fedha taslimu. Hali hii huibua changamoto nyingi zinazogusa pande zote abiria, makondakta na wamiliki wa vyombo vya usafiri. Ukosefu wa chenji husababisha usumbufu na malalamiko, huku wengine wakilazimika “kuachiana” chenji ndogo.
Upande wa wamiliki, changamoto kubwa ni kutokujua kwa uhakika mapato halisi yanayokusanywa kila siku. Wengi huishia kuweka utaratibu wa makisio, kwa mfano kumtaka dereva au konda kupeleka “elfu hamsini kwa siku,” bila kujua kama kiasi hicho kinaakisi uhalisia wa idadi ya safari na abiria waliopandishwa.
Wakati mwingine kiasi hicho kinaweza kuwa kidogo kuliko mapato halisi, au kikawa kikubwa kupita uwezo wa chombo kutokana na idadi halisi ya safari, hivyo kuleta upotevu au migogoro isiyo ya lazima, na mengine.
Kubadili mfumo wa malipo kuwa wa kidijitali kupitia kadi maalumu, huduma za simu za mkononi, au namba za QR, kunaweza kuleta manufaa mengi kuondoa changamoto hizo;
Fikiria mfumo ambao abiria wanalipia kwa simu zao. Kwa sekunde chache tu, muamala wa kidijitali unakamilika, nauli imelipwa, safari inaendelea. Hakuna tena mazungumzo ya “chenji sina,” wala konda kushika noti kuzikagua kwa wasiwasi wa kupokea “famba”, yaani noti feki.
Kwa upande wa mmiliki wa gari, taarifa za mapato zinapatikana moja kwa moja kupitia mfumo wa kidijitali; anajua kwa uhakika gari lake kutwa nzima limeingiza shilingi ngapi kiasi gani kwa siku, hana mashaka.
Mbali na simu, mfumo wa malipo unaweza pia kwa kadi, mtu ambaye anajijua daladala ni usafiri wake wa kila siku, anakata kadi maalum ya kumwezesha kusafiri, anaweka fedha taslimu, ya siku, wiki, mwezi, kulingana na anavyoweza, atapangusa tu kadi yake katika mfumo maalum wa kielektroniki ndani ya gari, tayari amelipia na safari imeanza. Jambo hili si nadharia lipo sehemu nyengine duniani.
Mfumo wa mabasi ya mijini katika mkoa wa Antalya, nchini Uturuki, unaendeshwa kwa mfumo wa kisasa unaoitwa Antalya Kart. Kila msafiri hununua kadi maalumu ya usafiri katika kituo, kisha huongeza salio kulingana na mahitaji yake. Basi linapowasili kituoni, abiria anapoingia ndani hupitisha kadi yake kwenye mashine ya kusomea papo hapo, nauli hukatwa na muamala hukamilika.
Mfumo huo umerahisisha utambuzi, kila daladala ina namba maalum, vivyo hivyo kila kituo. Hivyo, ukiwa unajua namba ya daladala, kwa mfano DC 15, unajua moja kwa moja kuwa inakufikisha hadi anapokwenda Mbagala Kizuiani bila usumbufu wa kuuliza au kuchanganyikiwa.
Aidha abiria kupitia aplikesheni maalum anaweza pia kujua sasa daladala anayosubiria iko wapi njiani na muda gani itafika kituo alichopo. Ni mfumo wenye nidhamu, urahisi, na uwazi unaorahisisha maisha ya wasafiri na watoa huduma kila uchwao mjini.
Hata hivyo, utekelezaji wa mfumo huu unahitaji ushirikiano wa wadau wote. Kwanza, mamlaka za usafiri kuweka miongozo ya pamoja kuhusu viwango na teknolojia zitakazotumika, ili kuhakikisha kuwa mifumo ya malipo na ile ya waendeshaji mabasi na inaoana na inaweza kufanya kazi kwa ufanisi.
Pili, ni muhimu kurasimisha mfumo mzima wa usafiri wa mijini. Mfano, utambuzi wa kila basi kwa namba au mfumo maalum, pamoja na utambuzi wa vituo vya kupandia na kushukia kwa mpangilio wa kimfumo. Hatua hii itamwezesha abiria kujua kwa urahisi anakopanda na kushukia kidijitali.
Tatu, upatikanaji wa huduma za mtandaoni kama intaneti ni sharti uwe wa uhakika. Mfumo wa kidijitali hauwezi kufanya kazi endapo mtandao unakatika mara kwa mara. Ili isitokee nauli imelipwa lakini unasikia “muamala haujafika”.
Nne, elimu kwa umma. Jamii inapaswa kuzoea kwenda sambamba na mabadiliko ya kisasa kwa kutambua kuwa matumizi ya huduma za fedha kidijitali si jambo la muda mfupi yamekuja kubaki nasi. Ni lazima tutilie mkazo ustaarabu. Ukweli kwamba malipo ya kwa mfumo huu wakati fulani inategemea hiari ya abiria, ufatiliaji ni mdogo, bila kusimamiwa, ambayo kama abiria hana utayari anaweza asilipie.