Dar es Salaam. Safari ya kunadi sera na kuomba ridhaa kwa Watanzania ili watoe nafasi kwa mgombea mmoja kati ya 18 wa urais kuiongoza Tanzania, imefika hatua za lala salama, baada ya kusalia siku 13.
Hatua hiyo, imefikiwa baada ya wagombea wa nafasi hiyo, kutumia siku 47 kunadi sera na kuomba ridhaa kwa Watanzania kupitia majukwaa ya kampeni, zilizoanza rasmi Agosti 28, mwaka huu.
Ndani ya siku hizo, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimefanya kampeni katika mikoa 27 na kuwafikia maelfu ya wananchi, kama ilivyo kwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), huku vingine vikifikia mikoa chini ya 15.
Katika dakika hizo za lala salama, kishindo cha kampeni kinatarajiwa kutimua katika mikoa zaidi ya 20, baadhi ya vyama vikitarajiwa kurudia katika maeneo ambayo tayari vimepita kujinadi.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, kipindi kilichosalia cha kampeni za urais, ndicho aghalabu huamua matokeo, kwa kuwa wananchi wanakumbuka sera za mwisho badala ya zile za awali.
Katika siku hizo 13 zilizosalia, Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kujinadi katika mikoa saba, ambayo ni Kagera, Rukwa, Katavi, Pwani, Dar es Salaam, Mjini Magharibi na atatamatisha Mwanza.
Kwa upande wa Salum Mwalimu wa Chaumma, atapiata kuomba kura katika mikoa saba ya Dodoma, Kigoma, Dar es Salaam, Morogoro, Tabora, Shinyanga na atatamatisha mkoani Simiyu.
Mgombea wa Ada Tadea, George’s Busungu atafanya kampeni katika mikoa sita ya Kigoma, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Mara na atatamatisha kampeni zake mkoani Mwanza.
Majaliwa Kyala anayegombea kwa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kwa siku hizo 13 atatamatisha kampeni zake katika mikoa sita ya Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na atafunga mkoani Dar es Salaam.
Kwa upande wa Mgombea wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Rwamugira Yustas atatembelea mikoa ya Kagera, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na atafunga kampeni zake mkoani Pwani.
Kunje Ngomaremwiru anayegombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wakulima (AAFP), katika siku hizo 13, atatembelea mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Tabora, Dodoma, Arusha, Tanga na atatamatisha mkoani Pwani.
Ingawa ratiba ya kampeni inaeleza hivyo, uzoefu unaonesha si vyama vyote vitakavyofanya mikutano ya kampeni katika mikoa kama ilivyopangwa.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Almas Kisabya amesema katika siku 13 hatatumia nguvu zaidi kuhitimisha kampeni zake, kwa kuwa alianza kwa kishindo na tayari ameeleweka.
“Tunaamini kwa jinsi tulivyofanya kampeni, kwa tulivyozunguka nchi nzima na kampeni tuliyoyafanya, visiwani, bara na maeneo yote, tunajivunia mambo mawili,” amesema.
Mambo hayo wanayojivunia, amesema ni kufanikiwa kutoa elimu ya kutosha kwa Watanzania kiasi cha kujua mipaka na mamlaka ya nchi yao.
Jambo lingine wanalojivunia kwa mujibu wa mgombea huyo ni kupata mapokezi makubwa katika mikutano yao ya kampeni, jambo linaloashiria wananchi watafanya uamuzi sahihi itakapofika siku ya uchaguzi, Oktoba 29, mwaka huu.
Amesisitiza kwa siku zilizobaki, watafanya kampeni ya rasharasha kwa sababu kazi kubwa imeshafanywa, wameimaliza na wananchi wamewaelewa vya kutosha.
“Tumeshafanya kazi kubwa, tunajiamini, kilichobaki tunawaachia wananchi wenyewe kuamua. Kazi imebaki kwa wananchi na kwa kuwa wametuelewa hatuna shaka watatupa nafasi zaidi,” amesema Almas.
Kwa upande wa mgombea urais wa United Democratic Party (UDP), Saum Rashid amesema wamejipanga kuzitumia siku hizo 13, kujihakikishia ushindi kwa maeneo yote waliyosimamisha wagombea ikiwemo ya urais.
Wanaamini ushindi kwa kile alichoeleza, wamezunguka maeneo mbalimbali kunadi sera zao, wananchi wamewaelewa, hivyo hawana shaka na uamuzi wa Watanzania itakapofika siku ya uchaguzi.
“Tunaamini tunashinda kwa sababu tunaona mwaka huu kumekuwa na tofauti katika usimamizi wa uchaguzi wenyewe. Tumeona tuna tume huru, sheria imara na matokeo ya kupatikana kwa wagombea mambo yalikuwa mazuri,” amesema.
Katika michakato ya mwaka huu, amesema hawakushuhudiwa kuenguliwa kwa wagombea katika chama chao, maeneo mengi wameteuliwa, wanafanya kampeni na wanasubiri hatua ya mwisho.
Amesisitiza yanayoendelea yanawapa matumaini ya ushindi, kwa kuwa kilichobaki ni juhudi zao kutengeneza mazingira ya ushindi.
“Kama tutaenda kama tulivyojiandaa na kujipanga, tunatarajia ushindi. INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), kuanzia mchakato wa uteuzi wa wagombea mambo yalikwenda vizuri,” ameeleza.
Amesema INEC iliwashirikisha kuanzia michakato ya awali kuelekea uchaguzi huo na kwamba hilo linawapa matumaini ya ushindi.
“Kwa namna tunavyoendelea, changamoto kwa asilimia kubwa ni rasilimali fedha kwa namna wagombea walivyojipanga, kwa hiyo tunatarajia kwa siku zilizobaki, kwenye maeneo tuliyojipanga vizuri tutashinda,” amesema.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia Makini, Coaster Kibonde amesema tayari kimejipanga kufanya kampeni za lala salama.
Kwa kuwa anatambua kampeni za lala salama zinakuwa na kishindo, ameeleza ameshajipanga kwa hilo, kwa kuhakikisha anayafikia makundi yote ambayo awali hakuwa ameyafikia.
“Tupo kwenye kampeni za lala salama kwa sasa nipo Kanda ya Ziwa na kuhakikisha nayafikia makundi yote. Keshokutwa nitaelekea mkoani Geita,” amesema Kibonde.
Amesema katika kampeni za lala salama, amejipanga kuhakikisha anakutana na makundi mbalimbali wakiwamo bodaboda kuwashawishi wakampigie kura na hatimaye atangazwe kuwa mshindi.
“Kampeni za lala salama zinakuwa na kishindo na tumekuwa tukipata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi na tumekuwa tukisikilizwa,” ameeleza.
Katika msisitizo wake kuhusu hilo, amesema amekuwa na uhakika wa kwenda kushinda katika uchaguzi huo, kwa kuwa ana vipaumbele na ahadi zinazokubalika na wananchi.
“Mimi siku zote nimekuwa na uhakika wa kwenda kushinda. Nakwenda kushinda na kwa kuwa vipaumbele na ahadi zetu zinawagusa moja kwa moja wananchi, kupitia hizo, tunaamini kwamba wananchi wametukubali na watakwenda kutuchagua Oktoba 29,” amesema Kibonde.
Katika mikutano yake ya kampeni za urais, Samia amesisitiza umuhimu wa wananchi kumpigia kura kwa wingi ili kukiheshimisha chama hicho na Tanzania kwa jumla wake.
Amesema wananchi wanapaswa kukichagua chama hicho kwa kuwa mgombea wake tayari ana uzoefu wa kuongoza, huku akiwapiga kijembe wapinzani wake kuwa, wakipewa nafasi watatumia muda mwingi kujifunza.
Samia amesisitiza kupewa ridhaa kwa chama hicho ni msingi wa kulinda kwa amani na kuuheshimisha utu wa Mtanzania, kwa kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo za afya, maji na nishati.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Majjid amesema kwa hatua za kampeni zilizosalia kunahitajika mbinu mbadala kutoka zile zilizotumika awali.
Amesema kama mgombea alianza kampeni kwa sera za kawaida, mwishoni watu watarajie kusikia maneno mazito, hoja nzito na wakati mwingine hadi zinazostua.
“Kama ulisikia sera ukasema zinachosha, mara nyingi nyakati za mwisho ndizo zinazotumika kueleza mambo mazito na ahadi nzito,” amesema.
Amesema utamu wa kampeni mara nyingi huonekana mwishoni, lakini ugumu wa uchaguzi husika ndio unaoamua mwisho uweje.
“Kwa mfano mgombea akijua ushindi wake uko hatarini iwapo hatafanya umaliziaji mzuri, basi kipindi kama hiki, anatumia kila mbinu kujenga ushawishi kwa wananchi wamchague,” amesema.
Majjid amesema katika nyakati kama hizo, ndipo unaweza kusikia masuala ya rushwa na ubadhilifu yakitajwa katika kampeni za vyama mbalimbali kikiwemo tawala.