Mwigizaji na mfanyabiashara maarufu Kim Kardashian hatimaye ameeleza kwa kina kilichomsukuma kuachana na rapa Kanye West, baada ya miaka minane ya ndoa.
Akizungumza katika kipindi cha “Call Her Daddy” kilichoongozwa na Alex Cooper, Kim, mwenye umri wa miaka 44, alisema kulikuwa na mambo mengi ambayo hakuweza kuvumilia tena kwenye ndoa yao.
“Sikupenda kuona mtu akiongea vibaya kuhusu watoto wangu, bibi yao au shangazi zao. Kama mtu anahisi hivyo, basi hatupaswi kuwa pamoja,” alisema Kim.
Kardashian alikiri kwamba hatua ya Kanye kufichua hadharani kuwa aliwahi kufikiria kutoa mimba wakati wa ujauzito wao wa kwanza ilikuwa moja ya mambo yaliyomuumiza zaidi.Pia aliongeza kuwa kutohisi usalama kihisia na kifedha kulimfanya aanze kufikiria upya uhusiano huo.
“Nilikuwa narudi nyumbani nakuta magari matano ya kifahari ya Lamborghini, kesho yake yamepotea. Alikuwa anayatoa kwa marafiki zake. Ukianza kuishi maisha ya kutotabirika hivyo, ni hali ya kutisha sana,” alisema.
Kim alieleza kuwa ukosefu wa uthabiti ulikuwa tatizo kubwa kwenye ndoa yao, jambo lililomfanya aogope kuendelea kuishi kwenye hali ya wasiwasi wa kila siku.
Licha ya hofu ya kutengwa katika ulimwengu wa mitindo na sanaa ambao Kanye alimuingiza, Kim alisema maamuzi yake ya kuachana na rapa huyo yalimfungulia milango mipya. “Miradi yangu mikubwa ilianza baada ya kufanya uamuzi huo. Niliona ulimwengu unanilipa kwa hatua sahihi niliyochukua,” alisema.
Kardashian pia alifichua kuwa moja ya sababu kuu za kufungua kesi ya talaka ilikuwa kutaka kuwa mfano bora kwa watoto wao wanne North (12), Saint (9), Chicago (7), na Psalm (6).
“Nilihitaji kujiokoa ili niwe mama bora. Nilihitaji kuwa thabiti kiakili ili niweze kuwalea vizuri,” aliongeza.