Dar es Salaam. Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa kushirikiana na AGRA na Mathematica Global imezindua warsha ya uhakiki wa tathmini ya uwezekano wa mabadiliko ya tabianchi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Lego la uhakiki wa tahmnini hiyo ni kuthibitisha ramani na taarifa muhimu za hatari za tabianchi ambazo zitasaidia Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kupanga mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo na mazingira.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, Mkurugenzi Mkaazi wa AGRA Tanzania, Vianey Rweyendela amesema mabadiliko ya tabianchi siyo jambo la nadharia tena, bali ni hali halisi inayoathiri maisha, uchumi na usalama wa chakula nchini.
“Tunahitaji kuacha kuangalia takwimu kama namba tu kwenye ripoti. Hizi ramani na data za hatari za tabianchi ni mwanga wa maamuzi kutoka katika upangaji na bajeti hadi utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema Rweyendela.
Ameongeza kuwa kupitia tathmini hii, AGRA na washirika wake wanaimarisha uwezo wa kitaasisi na jamii katika kutumia taarifa za kisayansi kupanga uwekezaji wa kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Kupitia ushirikiano huu, tunasaidia serikali na wadau kupanga mikakati ya kilimo kinachozingatia hali halisi ya tabianchi, kuimarisha uelewa, na kuongeza maandalizi kwa jamii zinazokabiliwa na hatari hizi,” amesisitiza Rweyendela.
Afisa Misitu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Timotheo Mande amesema Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) mwaka 1996, Itifaki ya Kyoto mwaka 2002 na Mkataba wa Paris mwaka 2018.
Ameeleza kuwa Serikali inasisitiza matumizi ya tafiti na data za kisayansi katika kupanga sera, bajeti na miradi ya maendeleo, kwani athari za tabianchi kama ukame, mafuriko, na kuongezeka kwa joto zinaathiri moja kwa moja uchumi na maisha ya wananchi.
“Serikali inataka kuona matokeo ya tafiti haya yanatekelezwa kwa vitendo ili kulinda maisha, uchumi na mazingira yetu. Tanzania ni yetu sote na tukiunganisha nguvu tunaweza kujenga taifa lenye ustahimilivu wa kweli,” amesema Mande.
Warsha hii ni sehemu ya mradi wa kikanda unaotekelezwa katika nchi tano Tanzania, Kenya, Uganda, Ghana, na Zambia ukiwa na lengo la kutoa ushahidi wa kisayansi unaosaidia watunga sera na wadau kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari za tabianchi, hasa katika sekta ya kilimo.
Kupitia ramani za hatari za tabianchi na zana za kidijitali za kuona takwimu, warsha hii inalenga kuweka msingi wa maamuzi yanayozingatia data kuanzia katika upangaji wa bajeti, miundombinu na uwekezaji wa kitaifa.
Tukio hilo limehudhuriwa na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Tari, Sua, NEMC, ASA, TOSCI, SAGCOT, Wizara ya Kilimo, ARU, UDSM, COSTECH, pamoja na mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
“Kwa pamoja tunaweza kubadili changamoto za tabianchi kuwa fursa za kujenga taifa lenye uchumi wa kijani, endelevu, na jumuishi,” amesema Rweyendela.