Waganga watakiwa kuwa na kamati ya maadili kudhibiti ramli chonganishi, mauaji

Geita. Wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kuanzisha kamati ya maadili ili kudhibiti waganga wasiosajiliwa ambao wamekuwa wakichafua taswira yao katika jamii na mauaji yatokanayo na ramli chonganishi.

Kupitia kamati hiyo, waganga wa tiba asili na tiba mbadala watakuwa na nguvu ya kuwadhibiti wataalamu wanaotumia ramli chonganishi na uchawi kuanzia ngazi ya shina mpaka mkoa, ikiwa ni pamoja na kuwashtaki katika Serikali na vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 16,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martini Shigella aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao kilichowakutanisha viongozi Chama cha waganga wa tiba asili nchini Tanzania (Tameso T), mganga mkuu wa Mkoa wa Geita na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela akizungumza katika Kikao kilichowakutanisha Viongozi wa Tiba asili na Tiba mbadala mkoani Geita

“Vizuri kuandaa kanuni zetu ili tuwadhibiti kwenye kamati zenu za maadili na kudhibitiana, waganga wetu wa tiba asili na tiba mbadala wanazidi kuongezeka, na huo mfumo unaweza kuwekwa kwenye sheria za nchi kama sehemu ya udhibiti kwa wasio waadilifu.”amesema Shigella.

Aidha Shigella amekemea baadhi ya waganga kutumia utaalamu wao na kuchukua maeneo ya wananchi, huku wakiwatishia kuwageuza chura, ambapo amewataka wenye tabia hiyo kwenda kufanya majaribio hayo kwenye kambi za Jeshi la Wananchi.

“Wako waganga ambao wanajitengeneza wanaenda kwenye kiwanja cha mtu wanaanzisha makazi, ukimfuata ukimwambia hapa ni kiwanja changu anakwambia nitakugeuza kuwa chura ondoka, akiulizwa anasema wakurugenzi wangu wameniambia tiba yangu ikae hapa.”

Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Waganga wa Tiba asili na Tiba mbadala mkoani Geita wakiwa katika Kikao leo Oktoba 16,2025.

“Nadhani ilee si kweli, kwa nini usiende katikati ya kambi ya Jeshi la Wananchi, mlishawahi kuona mganga amekwenda kukaa katikati ya kambi ya jeshi,”amesema na kuhoji Shigella.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,   Safia Jongo amewapongeza waganga hao kwa kuisaidia Serikali katika kudhibiti kupungua kwa matukio ya mauaji yatokanayo na ramli chonganishi ambapo mkoa huo ulikuwa juu kwa matukio hayo.

Pia Kamanda Jongo ameitaja changamoto ya ukosefu wa elimu ya kutosha namna ya kutofautisha wachawi na waganga wa tiba asili, kuwa chanzo cha matukio ya ramli chonganishi kuchochea sintofahamu katika jamii.

Mohamed Hamis,Mwenyekiti Waganga wa Tiba asili na Tiba mbadala wilaya ya Bukombe na Kaimu Mwenyekiti Kikao kilichowakutanisha Viongozi wa Tiba asili na Tiba mbadala Leo Oktoba 16,2025

‘’Kuna wanaojifanya waganga wa tiba asili lakini ni wachawi wanawaagiza wateja wao viungo vya binadamu na ushahidi wa matukio haya tunao, natamani tupite nyumba kwa nyumba tutoe elimu lakini pia tuwasajili’’ amesema Kamanda Jongo.

Aidha Kamanda huyo, ametoa wito kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala kutowaficha wale wanaopiga ramli chonganishi na wakitumia matatizo ya wateja wao kuwalaghai, huku wengine wakiwabaka hususani wanawake wanaofika katika vilinge vyao kupata huduma.

Mohamed Hamis ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Bukombe amesema kwa sasa wanajitahidi kutopiga ramli chonganishi kwa wateja wao, akisisitiza kuwa wanaofanya hivyo ni wachawi na washirikina wanaofanya mambo yao kwa kificho.