Dk Nchimbi ataja miradi ya Magufuli iliyomshtua, Samia akamshangaza

Dodoma. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema alishtuka miradi mikubwa ya Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ilipoanzishwa na akashangazwa ilivyokamilishwa.

Miradi hiyo ilianzishwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli na wakati ikiendelea kutekelezwa kiongozi huyo akafariki dunia na kijiti akakipokea Samia Suluhu Hassan aliyekuwa makamu wake wa Rais.

Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Siku mbili baadaye, Samia akaapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita.

Katika hotuba zake za mwanzo, Rais Samia aliahidi kuendeleza miradi yote ambayo ilianzishwa na mtangulizi wake na kuanzisha mipya. Miradi hiyo aliyoianzisha Magufuli, Samia ameikamilisha.

Leo Alhamisi, Oktoba 16, 2025 katika mkutano wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa mji mpya, Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, Dk Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza wa urais amewazungumzia hayati Magufuli na Rais Samia.

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amewanadi wagombea ubunge, George Malima wa Mpwapwa na George Simbachawene wa Kibakwe. Pia, amemwombea kura za urais, Samia na madiwani wote.

Dk Nchimbi amesema Watanzania wengi walikuwa na hofu na mashaka juu ya uwezo wa Rais Samia kama ataweza kuikamilisha miradi ambayo aliirithi kutoka kwa mtangulizi wake, hayati Magufuli.

“Watanzania wengi walikuwa na mashaka na hofu kwa sababu mabadiliko yoyote yanaleta hofu katika jamii. Miradi ambayo Mama Samia alianza nayo ambayo alirithi kutoka kwa Magufuli, Rais wetu aliyefariki dunia ilikuwa mikubwa sana.

“Nataka niwaambie, mimi binafsi wakati Rais Magufuli anaanza miradi mitatu mikubwa ya kimkakati, mradi wa umeme, mradi wa treni ya SGR, pamoja na mradi wa kuhamia makao makuu Dodoma, niliogopa, nikasema mzee huyu anatupeleka wapi ataweza kweli,” amesema Dk Nchimbi.

“Lakini mchakamchaka alioanza nao ulikuwa mkubwa, nyinyi ni mashahidi. Lakini alipofariki dunia tukasema sasa habari inakuwa ngumu zaidi, maana karibu yote mitatu ilikuwa haijakwenda mbali sana.”

Amesema lakini miradi hiyo ilikuwa imepiga hatua kubwa na Rais Samia katika hotuba yake ya kwanza, alilihakikishia Taifa nia na uwezo wa kuendeleza miradi hiyo anayo.

“Na kwa kweli kwa mafanikio makubwa, Rais Samia ameendeleza miradi hiyo na mmoja wa miradi ya kujivunia sana ni makao makuu ya chama chetu na makao makuu ya Serikali sasa yapo Dodoma,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema mambo makubwa yamefanyika Dodoma, ikiwemo upanuzi wa uwanja wa ndege ambao sasa ndege zinatua mchana na usiku. Vilevile Rais Samia amesimamia ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Msalato ambao sasa upo hatua za mwisho kukamilika.

“Amejenga heshima kubwa kwa chama chake, amejenga heshima yake yeye mwenyewe, amejenga heshima kwa Serikali na amejenga heshima kwa wanawake wote na kwa maana hiyo tumpe mitano mingine,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa.

Amesema wanakwenda kujenga vituo vipya vya afya vitano, zahanati mpya tisa na nyumba mpya za walimu 23, watajenga shule mpya za msingi tisa na za sekondari tano.

Amesema katika shule za zamani ili kuziwezesha kupokea wanafunzi wengi, watajenga madarasa 129 na nyumba za watumishi 21.

Eneo la kilimo, Dk Nchimbi amesema Ilani ya CCM imeeleza katika miaka mitano inayokuja wataendelea kuongeza bajeti ya kilimo katika shughuli za maendeleo.

“Pili, tutaendeleza ujenzi wa skimu za umwagiliaji ili watu wetu waweze kulima sio tu wakati wa mvua, lakini pia wakati wa ukame. Ruzuku ya mbegu na ruzuku ya dawa itaendelea kutolewa kwa wingi katika miaka mitano ijayo,” amesema.

Ili kuongeza upatikanaji wa maji Mpwapwa kutoka asilimia 66 hadi 80, Dk Nchimbi ameahidi miradi mbalimbali kutekelezwa ukiwemo wa Pwaga, Mungui, Itende Maswala.

Mradi mwingine ni wa maji wa Mugoma, Kata ya Godegode ambao unahusisha uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa matanki, mtandao wa mabomba na vituo vya kuchotea maji.

Eneo la barabara, Dk Nchimbi amesema ujenzi wa vivuko na madaraja, matengenezo makubwa ya barabara za Kidabaga, Nkololo, Muangalizi.

Amesema uwekaji wa taa za barabarani katika mji wa Mpwapwa na ujenzi wa barabara kiwango cha zege, barabara za Mapene, Mbuga, Idala, Lumuma, Tukuyu, Makose Junction na Idodi Dodoma.

Aidha, ukamilishaji wa barabara ya Kongwa hadi Mpwapwa kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa barabara ya Mpwapwa, Gulwe Chipogoro kilomita 75.

Kimbisa, Malisa na Pareso wasema…

Akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amesema mkoa huo ni nyumbani kwa CCM,

“Sasa kama CCM inatoka Dodoma, kwa hiyo lazima kila mwananchi ajitokeze kupiga kura, lazima tuongoze kwa kura, kwa sababu Mwenyekiti wetu (Samia) anakaa Dodoma, atapiga kura Dodoma.”

Kimbisa amesema mkoa huo utaongoza; “Namba mbili, namba tatu watashika Songea huko, namba nne au tano watashika Wahehe huko au Wasukuma, ili tuongoze lazima tujitokeze kwa wingi.”

Naye Mgombea ubunge wa Mpwapwa, George Malima amesema Serikali imefanya mambo mengi, walipokea Sh2.6 bilioni ambazo zilitumika kukarabati Hospitali ya Wilaya kwa kujenga jengo la mama na mtoto na la wagonjwa mahututi na zahanati tumejenga.

Malima anayetetea nafasi hiyo amesema wamejenga madaraja ya zege, Mpwapwa mjini wamejenga barabara ya lami kilomita tano, shule za msingi na sekondari.

Amesema miradi ya maji imetekelezwa lakini bado kuna maeneo hayajafikiwa na majosho yamejengwa.

“Tunaamini baada ya Oktoba, kuna mambo hayajakamilika ikiwepo barabara ya Mpwapwa kilomita 32 na thamani ya Sh51 bilioni, mkandarasi yupo, tunaomba mgombea mwenza utaweka msukumo,” amesema Malima.

Aidha, Malima amesema kuna kata nne za kimkakati hazijapata zahanati, hivyo ameomba hilo liangaliwe baada ya Oktoba 29, 2025.

Kwa upande wake, Kada wa CCM, Cecilia Pareso amesema chama hicho: “Ndiyo pekee kinachojua shida za Watanzania na namna ya kuzitatua.”

Pareso ambaye amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema amesema kupiga kura ni kujihakikishia maendeleo miaka mitano ijayo na kupiga kura ni uzalendo.