Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuufungua Mkoa wa Kusini Unguja kiuchumi na kiutalii, kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu, elimu, afya na uwezeshaji wananchi.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, katika uwanja wa Shule ya Paje, Mkoa wa Kusini Unguja, Dk Mwinyi amesema serikali itatekeleza miradi mikubwa katika maeneo manne makuu yatakayokuza uchumi wa mkoa huo.
Amesema miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa barabara kuu, madaraja mawili makubwa, viwanja vya ndege na barabara za ndani, ambapo maandalizi yake yako katika hatua za mwisho.

“Tunaendelea na ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tunguu hadi Makunduchi pamoja na madaraja makuu mawili yatakayounganisha Kusini na Mikoa ya Mjini na Kaskazini Unguja,” amesema mgombea huyo.
Amebainisha kuwa madaraja hayo yataunganisha Unguja Ukuu na Uzi pamoja na daraja la Chwaka, ambayo yatabadilisha sura ya mkoa huo na kuchochea maendeleo.
Aidha, amesema serikali itajenga bandari katika maeneo ya Kizimkazi na Mtende, sambamba na viwanja vya ndege vidogo vitakavyowezesha watalii kutua moja kwa moja Kusini Unguja.
“Tukishakamilisha miundombinu hii, uchumi wa Kusini Unguja utakua kwa kasi kubwa,” amesema Dk Mwinyi.
Katika sekta ya elimu, ameahidi ujenzi wa vyumba vya madarasa 2,000 vya shule za msingi na sekondari, ikiwemo shule za ghorofa 10 za sekondari na shule za ghorofa kwa ngazi ya msingi.
Kuhusu afya, amesema serikali itajenga hospitali kuu mbili kubwa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Saratani na Hospitali ya Kufundishia katika eneo la Makunduchi.
“Hapa tutakuwa tumekamilisha huduma za afya kwa kiwango cha juu kabisa,” amesisitiza.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi akizungumza na Wananchi, wanachama na wafuasi wa chama chama hicho katika mkutano wa kampeni uwanja wa Shule ya Sekondari Paje Mkoa wa Kusini Unguja
Akigusia changamoto ya maji, Dk Mwinyi amesema ipo miradi mikubwa yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 ambayo itamaliza kabisa tatizo hilo mara itakapokamilika.
Katika eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi, alisema serikali itatekeleza mikakati minne muhimu: kutoa elimu, kuongeza mikopo, kuboresha miundombinu na kutafuta masoko kwa bidhaa za wananchi.
Aidha, ameahidi kuongeza ajira serikalini, hasa katika vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), na kuweka mazingira bora kwa sekta binafsi ili kuajiri vijana zaidi.
“Kipekee tutaendeleza miradi ya kilimo, uvuvi na ujasiriamali kwa vijana. Mipango ipo tayari na utekelezaji umeanza,” amesema.
Kuhusu utalii, amesema eneo la Paje ni kitovu cha shughuli hizo hivyo serikali itahakikisha linaendelea kuwa na mazingira mazuri kwa wawekezaji na vijana wanaofanya kazi katika hoteli na kampuni za utalii.
Dk Mwinyi amesisitiza kuwa amani na maridhiano ya kisiasa yaliyodumu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yaliyopatikana Zanzibar.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, alimnadi Dk Mwinyi akimwelezea kama kiongozi anayechukia rushwa na ufisadi, na ambaye ameonyesha ufanisi mkubwa katika uongozi wake wa miaka mitano.
“Dk Mwinyi amekuwa kinara wa maendeleo na kiongozi asiyevumilia vitendo vya rushwa. Tunawaomba wananchi wampe tena ridhaa aendelee kuleta maendeleo zaidi,” amesema Dk Dimwa.