Pemba. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar atailinda heshima ya mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Katika kauli yake hiyo, amesema Wazanzibari watakapomchagua Rais wa sasa atakuwa mstaafu, hivyo atahakikisha anailinda heshima yake kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya Zanzibar.
Othman ameyasema hayo leo, Alhamisi Oktoba 16, 2025 alipohutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Skuli ya Pandani, Pemba katika mwendelezo wa kampeni za urais visiwani humo.
Amesema atakaposhinda nafasi ya urais visiwani humo, atalinda heshima ya Rais mstaafu, sio kwa sababu hakumkosea, bali kwa sababu ameamua kuwa mstaarabu.
“Nitakapokuwa Rais, nitatimiza matakwa ya Katiba yetu, inayosema Rais aliyepo na Serikali ilinde heshima ya Rais mstaafu. Tutatimiza masharti hayo kwa sababu sisi ni waungwana si kwa sababu hukutukosea,” amesema.
Licha ya ahadi hiyo, amesema ulinzi huo wa heshima kwa atakayekuwa rais mstaafu hautahusisha kuacha kushughulikia matendo yoyote ya ubadhilifu wa fedha za umma.
“Isipokuwa moja tu, kama kuna makaburi yamezikwa, mna fedha zetu, hayo tutayafukua tutoe fedha tu hatufanyi jambo lingine,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, Othman amesema kuna umuhimu kwa Serikali kuzipa sauti za wananchi nafasi kwani kufanya hivyo, kutaiangamiza nchi.
Amesema bila kujali kutakuwa na vitimbi kiasi gani ni vema wananchi wajitokeze kwenda kupiga kura ili kushinda nafasi hiyo.
Atakaposhinda, amesema atahakikisha anarudisha haki ya nchi kwa wananchi, ili wawe na mamlaka kamili na hatimaye kujiinua kiuchumi.
Lingine, amesema atafanya kila namna kuondoa njaa katika visiwa hivyo kwa kushusha bei ya chakula ili kila mtu aweze kula na familia yake.
“Watoto wetu waweze kula bila kupata udumavu. Tunataka kuhakikisha chakula kinashuka bei ili kila mtu aweze kula na familia yake,” amesema.
Ameeleza atafanya hivyo kwa kuondoa ushuru, ada, tozo, kodi kuanzia kwa maziwa ya mtoto na vitu vingine vyote vinavyohusu chakula.
“Isipokuwa soda tu, kwa sababu hiyo ni anasa yako. Na sisi hatukwambii unywe soda matunda yote yaliyojaa hapa, kunywa juisi ya matunda,” amesema.
Ameahidi kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa viwango vya hali ya juu, ili wananchi wapate matibabu ya kibingwa kwa gharama nafuu na maeneo ya karibu.
Othman amesema anatarajia kusherehekea miaka 85 ya elimu Pandani, kwa kuwa ndio kongwe zaidi na ilianzishwa mwaka 1942.
Hata hivyo, ameahidi kujenga skuli ya kisasa kuakisi ukongwe wa eneo hilo kielimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amewasisitiza wananchi kukichagua chama hicho kwa kuwa kina dhamira ya dhati ya kuwaongoza kwa haki.
Amesisitiza ni chama hicho pekee ndicho kinachojua changamoto na shida wanazokabiliana nazo wananchi, hivyo hawana budi kukichagua.