Miili minne yaokotwa kando ya barabara, Polisi yachunguza

Kibaha. Jeshi la Polisi mkoani Pwani linachunguza tukio la kutatanisha baada ya miili ya watu wanne kukutwa kando mwa barabara ya kutoka Mapinga kuelekea Kibaha, katika maeneo ya Kidimu–Vingunguti, wilayani Kibaha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema miili hiyo iligunduliwa baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kidimu kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

“Baada ya taarifa kupokelewa, kikosi cha askari polisi kikishirikiana na wataalamu wa uchunguzi wa makosa makubwa kilifika eneo la tukio na kukuta miili ya wanaume wanne waliokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 19 hadi 22,” amesema Kamanda Morcase.

Amesema watu hao hawakuwa na vielelezo vya utambulisho na walikutwa na majeraha usoni na kwenye miguu, ishara kuwa huenda walipigwa au kuteswa kabla ya kufariki dunia.

Amesema miili hiyo ilipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi zaidi wa kidaktari, hata hivyo, kamanda huyo amesema tayari miili hiyo imeshatambuliwa na ndugu zao.

Waliofahamika ni Mikidad Mikidad (21) na Hassan Jumanne (21), wote wakazi wa Tabata Chang’ombe na madereva bodaboda; Fadhil Hiyola (19), mkazi wa Vingunguti Miembeni na Abdallah Nyanga (21), dereva  bajaji mkazi wa Tabata Kisukuru jijini Dar es Salaam.

Amesema tyari miili hiyo imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo na wahusika wa mauaji hayo na limewataka wananchi wenye taarifa zozote muhimu kujitokeza kusaidia kufanikisha uchunguzi huo.

“Tunaomba ushirikiano wa wananchi. Taarifa yoyote muhimu itapokelewa na kuchukuliwa hatua za haraka,” aliongeza Morcase.

Tukio hili limezua taharuki kwa wakazi wa Kibaha na maeneo ya jirani, huku baadhi wakihusisha hali hiyo na matukio kadhaa ya uhalifu yaliyowahi kuripotiwa katika mkoa huo miezi ya karibuni. Mwaka jana, matukio ya miili kupatikana kandokando ya barabara yameripotiwa katika maeneo ya Mkuranga na Kongowe, ingawa chanzo chake hakikuwahi kubainishwa wazi.

Wakazi wameshauri vyombo vya dola kuongeza doria na kufuatilia kwa karibu mitandao ya wahalifu ili kuzuia matukio kama haya kujirudia.